22 July 2013

MBOWE AWAPA SOMO WATANZANIA Na Suleiman Abeid, Shinyanga
CHAMA Ch a Demo k r a s i a na Maendeleo (CHADEMA) kimewaomba Watanzania kuweka pembeni tofauti zao za vyama vya siasa, dini na ukabila na waungane kujadili mustakabali wa nchi yao, huku kikisisitiza suala la kuwajengea ukakamavu vijana wake wa Red Brigade.Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alipokuwa akihutubia umati wa watu katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa.Mbowe alisema kuna kila sababu ya Watanzania kuungana pamoja na kukaa chini ili kujadili mustakabali wa nchi inavyokwenda. Alisema kwa sasa kuna viashiria vinavyoashiria amani na utulivu kupotea.

"Sisi CHADEMA tunasema hali ya mambo yanavyokwenda hapa nchini siyo nzuri, kuna kila sababu ya kukaa chini tuangalie tulikotoka, wapi tulipo na huko tunakokwenda, na hii tusitangulize mbele itikadi za vyama vyetu vya siasa, udini au ukabila, CHADEMA tunasema daima tutahubiri amani, nchi yetu sasa hivi inakabiliwa na matatizo mengi, tutafute jinsi gani tutamrejea Mungu ili hali ya amani iweze kuimarika, tusiangaliane kwa itikadi ya vyama vya siasa wala dini," alisema Mbowe.Akizungumzia tukio la Arusha, mwenyekiti huyo alisema viongozi wote wa CHADEMA waliokuwa katika mkutano ulioshambuliwa kwa kurushiwa bomu walinusurika kifo kutokana na mipango ya Mungu ambapo alisema washambuliaji katika tukio hilo walitumia aina nne tofauti za silaha.
"Tukio la Arusha kusema kweli tulinusurika kwa mapenzi ya Mungu, maana tulishambuliwa kwa silaha nne tofauti, kwanza kwa bomu liliua watoto na wanawake, kisha zikafyatuliwa risasi za moto kwa kutumia SMG, lakini tukapigwa bastola, na tulipojaribu kuokoa majeruhi tukapigwa mabomu ya machozi," alisema Mbowe.Aliongeza kuwa; "Polisi tuliotegemea watulinde wote walikimbia kuondoka katika eneo la tukio, hivyo tunaposema tutawajengea ukakamavu vijana wetu wa Red Brigade, wenzetu CCM wasituelewe vibaya wala wasiogope, CHADEMA hatuhitaji jeshi la kutumia silaha, tunataka ulinzi kwa viongozi wetu na kwenye shughuli zetu za chama, kama wanavyofanya CCM wenyewe kupitia vikundi vya Green Guard."
Katika kuthibitisha kuwa CCM inavyo vikundi vya Green Guard, Mbowe alionesha hadharani kitabu cha Sera na misingi ya CCM ambacho ndani yake kinaelekeza masuala ya kuwajengea uwezo vijana wake na waweze kupambana na vijana wa vyama vya upinzani.Hata hivyo alisema iwapo Watanzania watakataa chama hicho kisiwe na kikosi hicho wao wako tayari kuachana na mpango huo na kama wataruhusiwa wataendelea kuwajengea ukakamavu vijana wao kwa nia nzuri ya kuweka ulinzi katika shughuli zote za CHADEMA.Aliwataka wapenzi na wanachama wa CHADEMA kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao kwenye mabaraza ya katiba ambapo alisema chama chake kinaunga mkono suala la uwepo wa Serikali Tatu.

No comments:

Post a Comment