22 July 2013

MAJAMBAZI YATEKA TENA BASI LA ABIRIA Na Abdallah Amiri, Igunga
KUNDI la watu 20 wanaodhaniwa majambazi wameteka basi la kampuni ya Mohamed Trans Ltd lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba katika tukio lililotokea katika Kijiji cha Igogo Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora.Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, zilieleza kuwa baada ya abiria wa basi hilo kufika eneo la Igogo walikuta majambazi hao wamepanga mawe na magogo katikati ya barabara na ndipo dereva ililazimika kusimama.

Baada ya kusimama majambazi hao walianza kulishambulia kwa mawe na kuamuru kondakta wa basi hilo awashushe abiria, amri ambayo aliitekeleza.Habari kutoka polisi zilieleza kuwa basi lililotekwa ni lenye namba T840 AVW lilikuwa na abiria 60. Tukio hilo lilitokea juzi saa tano na robo usiku. Baada ya basi hilo kutekwa basi jingine la kampuni ya Summry lenye namba T 620 BEW lililokuwa likiendeshwa na Moses Tindua (40), mkazi wa jijini Dar es Salaam ambapo lilikuwa limesindikizwa na askari wawili likitokea Bukoba kuelekea Jijini Dar es Salaam lilifika eneo hilo na ndipo polisi walishuka na kuanza kurusha risasi hewani na majambazi hao kufanikiwa kukimbia.
Askari waliofanikiwa kuokoa abiria hao ni D 8105 PC Josephat na H 1476 PC Athumani wote wa Kituo cha Polisi wilayani Igunga.Askari hao waliongeza kuwa kutokana na mwanga wa gari majambazi waliweza kuwaona na kufanikiwa kukimbia. Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Wilaya ya Igunga, Abeid Maige, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hakuna abiria aliyeibiwa wala kujeruhiwa.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea kuwasaka majambazi hao na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano ili waweze kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Hilo ni tukio la pili ndani ya kipindi cha mwezi huu, ambapo hivi karibuni majambazi 10 yakiwa na silaha za kivita yaliteka mabasi mawili yaliyokuwa yakitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam na Arusha kwenye pori la Biharamulo.

No comments:

Post a Comment