14 December 2010

Chove azidi kumtesa Kilinda

Na Addolph Bruno

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya JKT Ruvu, inayoshiriki Ligi Kuu Bara, Charles Kilinda, amesema kuondoka kwa kipa Jackson Chove aliyekwenda Azam FC, ni pengo kubwa kwa timu yakeKipa huyo alisajiliwa na Azam mwanzoni mwa msimu wa
ligi akitokea JKT pamoja na Mrisho Ngassa aliyetokea Yanga.

Akizungumza na Majira kwa simu jana, Kilinda alisema nafasi iliyoachwa wazi na kipa huyo, bado ni tatizo na alipanga kuiziba katika dirisha dogo la usajili, lakini amekosa kipa mwenye kiwango.

"Chove alikuwa ni kipa mzoefu,  alipoondoka na kujiunga Azam FC,  sina kipa mzoefu, sijalipatia ufumbuzi na usajili umemalizika," alisema.
Kilinda aliongeza kuwa, kwa sasa amebakiwa na kipa mmoja anayemtegemea Shaaban Dihile, lakini anahitaji msaada kutoka kwa kipa mwingine.
Kocha huyo alisema kikosi chake kinaanza mazoezi ya nje ya kambi leo kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu baada ya kumaliza likizo ya wiki tatu waliyopewa.

Alisema mzunguko wa pili unatarajia kuwa mgumu,  kutokana na mzunguko wa kwanza kuwa na upinzani mkubwa na kupishana kwa pointi kidogo.

Katika msimamo wa ligi hiyo, JKT ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa sita kwa kujikusanyia pointi 14.

No comments:

Post a Comment