22 July 2013

MBUNGE ATOKWA MACHOZI MKUTANONI Na Yusuph Mussa, Korogwe
FITINA za kisiasa zimemfanya Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM) Stephen Ngonyani (Profesa Majimarefu) kushindwa kuwahutubia wapiga kura wake kwenye mkutano wa hadhara na kuanza kutokwa machozi baada ya kubaini baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye jimbo hilo wamemchonganisha na Mwenyekiti wake Taifa, Rais Jakaya Kikwete.

Viongozi hao wa chama chake walivitumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe kwa Rais Kikwete kwa kusema Mbunge huyo na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo wanawapendelea zaidi wakulima kuliko wafugaji, ndiyo maana hata baada ya tukio la kuchomwa nyumba 16 za wafugaji wa kitongoji cha Chang'andu mapema mwaka huu, wachomaji hawakuchukuliwa hatua.
Hali hiyo ilimtokea Ngonyani mwishoni mwa wiki ambapo akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, ambaye alifika Kijiji cha Magamba- Kwalukonge kuzungumza na wananchi tangu mkasa huo utokee hivi karibuni, Gallawa alimtaka Ngonyani kuzungumza na wananchi wake.
Ngonyani alisema baadhi ya watu wamesema anawapendelea wakulima kuliko wafugaji na kufikia hatua ya 'kuwashtaki' yeye na Mkuu wa Wilaya kwa Rais Kikwete, na kusema sio kweli kwamba anawapendelea wakulima, bali wote ni wapiga kura wake na baada ya kutokea kwa maafa hayo ya kuchomewa nyumba walifika mara kadhaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiwa ni pamoja na kutoa vyakula kwa waathirika hao.
"Kuna watu wamenichonganisha na Rais wangu kuwa napendelea wakulima kuliko wafugaji, hilo sio kweli,kwani kipindi chote cha matatizo yao..." alisema Ngonyani. Hata hivyo alishindwa kuendelea na kwenda kukaa nyuma ya jukwaa huku akibubujikwa na machozi.
Gambo alisema wote ni wananchi wao, lakini suala la wafugaji kuingiza mifugo na kula mahindi karibu ekari sita ni kuwaonea wakulima.
Alisema hata waliochoma nyumba hawakuwa sahihi ndiyo maana waliamua kuwatuma wataalamu wa ardhi na kwenda kupima matumizi bora ya ardhi kwenye Kijiji cha Magamba- Kwalukonge na hali ya amani imerejea.
Mwananchi mmoja, Valentine Fwalo alimuelza Mkuu wa Mkoa mpango wa matumizi ya ardhi huenda ukakwama baada ya baadhi ya wafugaji kukata kwa mapanga vibao vinavyoonesha mipaka ya wakulima na wafugaji  

No comments:

Post a Comment