Esther Macha
WAJIBU na majukumu ya Madiwani ndani ya
Halmashauri nchini ni kuwahudumia wananchi ili wajiletee maendeleo na pia
kulenga kumwezesha diwani kuwa na fikra na mitazamo chanya katika ushirikiano
wake na jamii.Wajibu wake
utampasa kuwa kiongozi mwenye mwenendo wa kimaadili, mtazamo wa kifikra kuhusu
juhudi za kazi, uzalendo, kujitegemea, udumishaji wa mshikamano wa jamii na
umoja wa kitaifa katika kuendeleza amani na utulivu.
Hata hivyo,
sifa za uongozi kidemokrasia katika uhamasishaji na kujenga uwezo wa jamii na
stadi muhimu za mawasiliano na usuluhishi wa migogoro zimeelezwa ili kumjengea
diwani sifa, uwezo na uhalali katika kutimiza majukumu yake.
Suala la uwazi
na uwajibikaji katika kutimiza mahitaji ya ibara ya 8 ya Katiba imezingatiwa
kwa kuelezea mifumo na taratibu zilizopo na kuonyesha nafasi zake katika kukuza
dhana ya Uwazi na uwajibikaji.
Ili kuweza kutimiza hayo hivi
karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ilifanya ziara ya
kimafunzo wilayani Kilombero mkoani Morogoro lengo likiwa ni utekelezaji bajeti
ya mwaka wa fedha 2012/13 kupitia mradi wa kuwajengea uwezo madiwani nchini.
Mafunzo hayo ni
nyenzo muhimu kwa madiwani wote ili waweze kupata mafunzo ya kiutendaji pamoja
na kupata uelewa juu ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika kata zao.
Lengo kuu la
ziara hiyo ni ukusanyaji wa mapato yatokanayo na mchele,utatuzi wa migogoro ya
wakulima na wafugaji, uhifadhi wa mazingira misitu na vyanzo vya maji, kilimo
uzalishaji wa mpunga.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Bw.Kenneth Ndingo anasema kuwa lengo la ziara
hiyo ya kimafunzo ni kubadilishana uzoefu na wilaya hiyo ya Kilombero kwani
historia ya mahusiano ya kilimo na hali ya hewa inafanana .
"Unajua
wilaya hii inafanana vitu vingi sana
na Wilaya yetu ya Mbarali hivyo tuliona ni vema kuja kujifunza huku tujue
wenzetu wanafanyaje kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji na hata upatikanaji
wa mapato kwenye kilimo cha mchele," anasema Bw. Ndingo.
Hata hivyo,
hatua waliyoanza nayo madiwani ni kutaka kujua utatuzi wa migogoro katika Wilaya
ya Kilombero kama uongozi wa halmashauri
wanatatua vipi. Diwani wa kata ya Luhanga, Bw.Baraka Leteyo alitaka kujua
operesheni ya kupunguza mifugo Kilombero na idadi inayotakiwa kubaki kama
wanyama kazi na kujibiwa kuwa wanyama wanaotakiwa kubaki ni nane wanaruhusiwa
kubaki kama wanyama kazi na si zaidi.
Diwani mwingine
wa Kata ya Ruiwa Bw. Alex Mdimilaje anasema kuwa walichoweza kujifunza katika
ziara hiyo ni pamoja na wafugaji wa eneo hilo
kuunda umoja wao ambao unawasaidia kutatua kero zao.
Bw. Mdimilaje
anasema kuwa umoja huo pia unawasaidia kubaini wafugaji wanaoingia kinyemela
wanaotoka mikoa ya jirani kuvamia Wilaya ya Kilombero baada ya mikoa waliyotoka
kuhamishwa kinguvu.
"Pia
kupitia umoja wao wanaweza kukopesheka katika taasisi mbali mbali za kifedha
hivyo ni vema na sisi wilaya yetu ya Mbarali tukafanya mazungumzo na wafugaji
wetu ili nasi tuweze kuwa na vitu kama
hivi." anasema Diwani huyo.
Akizungumzia utatuzi huo wa migogoro,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Bw.Daudi Ligazio anasema kuwa
mbinu zinazotumika kukabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji ni kuweka
alama za mifugo,upimaji wa ardhi ya malisho,wafugaji kuwekewa kadi maalumu ya
utambuzi, jumla ya vijiji 71 vimepimwa na kuwekewa mpango wa matumizi bora ya
ardhi kati ya hivyo vijiji 24 vimepimwa kwa ajili ya ufugaji.
Hata hivyo, anasema kuwa wilaya ya
Kilombero katika utatuzi huo wa migogoro wilaya ilihamisha mifugo 202,752 kati
ya mifugo 24,578 iliyohamishwa kwa shuruti,mifugo 53,168 iliuzwa minadani na
jumla mifugo 125,000 ilitoroshwa kupitia njia za panya.
Kitu kingine ambacho waliweza kujifunza
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mbarali ni ukusanyaji wa mapato ambapo
halmashauri ya Wilaya ya Kilombero inatumia watendaji wa kata katika ukusanyaji
wa ushuru tofauti na Wilaya ya Mbarali ambapo inatumia mawakala kukusanya
ushuru huo.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw.
Ligazio anasema kuwa ili kuweza kuboresha ushuru huo halmashauri hutoa motisha
kwa watendaji wa kata, pia halmashauri imeunda timu ya ufuatiliaji wa mapato
ambayo wajumbe wake hubadilishwa mara kwa mara na mwenyekiti wake akiwa ni
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Bi.Azimina Mbilinyi.
Kwa upande wake mweka hazina wa
halmashauri hiyo, Bw.Mbwana Msangi anasema kuwa ili kuboresha mapato, halmashauri
inatengeneza vitabu vyake vya ushuru kutoka Mpigachapa Mkuu wa Serikali ili
kupunguza wizi utokanao na vitabu bandia na kila tarehe 15 ya mwezi lazima
wanahakiki vitabu.
Akizungumzia kuhusu wazabuni mweka
hazina huyo anasema kuwa hawajaweza kuwapa wazabuni kazi ya ukusanyaji ushuru
mpaka pale watakapojiridhisha kwa kutembelea wilaya zingine kujifunza.
"Mikoa na wilaya ambazo tumeweza
kutembelea kujifunza ni Jiji la Mwanza, Shinyanga, mapato yetu ya ndani ni
wanayokusanya watendaji ni bil.3 kwa mwaka na kwamba hadi kufikia Juni mwaka
2013 ushuru wa mazao, nafaka watakuwa wamekusanya sh. bil.1.4," anasema
Bw. Msangi.
Hata hivyo, anasema kwa wale wanasiasa
ambao wana tabia ya kuchochea wananchi kutolipa ushuru mbalimbali kuwa Ofisi ya
Mkurugenzi wa Wilaya huchukua hatua ikiwemo suala hilo kuingizwa kwenye vikao na kumwomba
diwani wa eneo husika kuacha uchochezi huo mara moja.
Kwa upande wake Ofisa kilimo na Takwimu
Wilaya ya Mbarali Bw.Vanscar Kulanga alitaka kujua kama
halmashauri ya Kilombero inatoza ushuru kwa kuzingatia vipimo vya uzito au
ukubwa na lumbesa wanadhibiti vipi.
Kwa upande wa mweka hazina Wilaya ya
Kilombero anasema kuwa, halmashauri inapambana na rumbesa kwa kutoza adhabu ya
malipo zaidi ya kwa kila mfanyabiashara anayebainika kujaza lumbesa na baada ya
kulipa adhabu huwa wanaamriwa kujaza upya kwa kuzingatia magunia yenye ujazo wa
kilo 100.
Kwa upande wake Kaimu Mk u r u g e n z
i Mt e n d a j i wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Bi.Tyatawelu Mongo alitaka
kujua ada za wanafunzi wa sekondari zinakuwa chanzo cha mapato ya halmashauri.
Mweka hazina Wilaya ya Kilombero
anasema kuwa rekodi zote zinaingizwa kwenye vitabu vya halmashauri na
kuwasilishwa kwenye vikao ila fedha hizo huwa zinabaki katika shule husika kwa
mwongozo wa TAMISEMI.
Ziara hiyo ya kimafunzo ya madiwani wa
halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ilikuwa ya siku tano ambayo lengo
lake ni utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa
fedha wa 2012/13 kupitia mradi wa kujenga uwezo (Capacity Building Grant).
Hata
hivyo, ziara hiyo iliongozwa na wakuu wa idara mbalimbali wa halmashauri hiyo
ikiwemo fedha, kilimo, mazao, maliasili,mifugo pamoja na mipango miji.
No comments:
Post a Comment