23 July 2013

MAONESHO YA NANENANE HATI HATI KUFANYIKA Na S e v e r i n B l a s i o , Morogoro

MFUMO mpya wa mtandao wa kutoa fedha za Serikali 'epical' huenda ukasababisha maonesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki kuahirishwa hadi Septemba kutokana na halmashauri husika kuchelewa kutoa mchango wa kufanikisha shughuli hiyo. Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha kutathmini michango ya sherehe hizo kilichofanyika katika ofisi zao zilizoko Nanenane mjini humo.

Kwa mujibu wa Katibu wa TASO, Kanda ya Mashariki, Rafael Majivu alisema mpaka Julai19 mwaka huu halmashauri walikuwa wamechangia kiasi cha shilingi milioni 7 wakati sherehe kwa ujumla inahitaji shilingi milioni 112. Kutokana na hilo wajumbe wa kikao walishauri ni vyema waahirishe maonesho hayo mpaka Septemba mwaka huu ili halmashauri zijiadae vizuri.
''Mheshimiwa mwenyekiti tunaona kuna sintofahamu kwa sababu hiki si kikao cha kwanza katika kuweka mikakati... sherehe ni mwezi ujao hakuna pesa yoyote ni bora sherehe yetu ya Nanenane tuipeleke mwezi Septemba," walipendekeza baadhi ya wajumbe. Walilalamika wakurugenzi na wakuu wa wilaya kwa kukaa kimya bila kushughulikia suala hilo kwa kisingizio cha mtandao, wakati wanavyo vyanzo vingi vya kupata pesa katika halmashauri zao.
Katibu tawala msaidizi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Lameck Noah aliwashauri wakurugenzi kutafuta fedha nyingine ili kuhakikisha wanachangia kufanikisha shughuli hiyo. ''Nadhani ndugu zangu wajumbe fanyeni juu chini mkamilishe michango...leo hii tupo nyuma na wakati... tafuteni vyanzo vingine kama vile kukopa kwenye ushuru wa mazao ambapo mtarudisha baadaye fedha hizo,'' alisema Noah.

No comments:

Post a Comment