Na Said Hauni, Lindi
WAKAZI wawili wa mji mdogo wa Masoko, Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi
wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya
heroine na bangi kete 35.
Kwa mujibu wa
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Renata Mzinga, wakazi hao wamekamatwa
katika msako uliofanywa Juni 29, mwaka huu saa 3:30 usiku.
Mzinga aliwataja waliokamatwa kuwa ni
Abdullah Abdallah (30) na Mohamedi Maulidi Meli (18), wote wakazi wa mji mdogo
wa Masoko, Wilaya ya Kilwa.
Alisema Abdallah alikamatwa eneo la Mkapa
Garden akiwa na dawa za kulevya aina ya heroine gram mbili na mabomba matatu ya
sindano yaliyokuwa yakitumika kujidungia.
Pia alisema Maulidi alikamatwa maeneo ya
Shule ya Sekondari ya Kilwa akiwa na kete 35 za bangi ambayo alikuwa akiitumia
kwa biashara.
Mzinga ameliambia gazeti hili kwamba
watuhumiwa wote wawili tayari wameshafikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo ya
Kilwa kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kaimu kamanda huyo wa polisi aliwaomba wananchi
kushirikiana na jeshi hilo katika kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo
ambavyo kimsingi havileti maendeleo mazuri kwa jamii.
No comments:
Post a Comment