SERIKALI ya Marekani kupitia ubalozi wake nchini
umepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wakati wa
ziara ya Rais wa nchi hiyo, Barack Obama, anaripoti Mwandishi Wetu.
Wakati wa ziara ya Rais
Obama, TTCL ilipewa dhamana ya kusimamia mawasiliano tangu akifika kiongozi
huyo hadi kuondoka. Baadhi ya maofisa kutoka ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini
wakiongozwa na afisa wa ubalozi huo, Jeff Shrader, walifika makao makuu ya
kampuni hiyo Jumatano wiki hii ambapo walikutana na uongozi pamoja na
wafanyakazi waliohakikisha kuwa suala zima la mawasiliano linakwenda vizuri na
kwa ufanisi.
Mkuu wa Masoko na Mauzo wa
TTCL, Peter Ngota, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa kampuni hiyo imepata
faraja kubwa kwa kupata mrejesho huo kutoka serikali ya Marekani.
“Tumepata faraja hii
inaonesha uwezo wetu kitaaluma na ubora wa vifaa tulivyo navyo katika kutoa
huduma za mawasiliano,” alisema.
Alisema TTCL ilipewa sifa
hasa kutokana na utaalamu, uchapa kazi na weledi wa hali ya juu uliooneshwa na
wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa timu ya Wamarekani waliokuwa wanafanya nayo
kazi.
Wafanyakazi na viongozi
kadhaa wa TTCL walipewa zawadi mbalimbali kama
njia ya kutambua mchango wao.
Ngota alisema kuwa kampuni
hiyo itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha kuwa inakuwa mtoa huduma bora wa
kimataifa wa mawasiliano hapa nchini.
Ujumbe huo wa Wamarekani
umeahidi kutoa vyeti vya kutambua mchango wa TTCL na wafanyakazi wake katika
siku chache zijazo.
Kampuni hiyo ya simu
inaendesha na kusimamia mkongo wa taifa wa mawasiliano kwa niaba ya Serikali ya
Tanzania
kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
No comments:
Post a Comment