Na Rehema Mohamed
HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
leo inatarajiwa kutoa Hukumu ya kesi inayowakabili Wakurugenzi wa Kampuni ya
Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), iliyokuwa
ikijihusisha na kuendesha na kusimamia mchezo wa upatu.Kesi hiyo
inawakabili wachungaji wa makanisa tofauti ya Pentekoste, ambao ni Jackson Mtares, Dominic
Mtares, Timotheo Ole Loitingye na Arbogast Francis.
Hukumu hiyo
inatarajiwa kutolewa leo mahakamani hapo mbele ya Hakimu Stuwarti Sanga,
aliyekuwa akisikiliza shauri hilo
ikiwa takriban miaka minne imepita tangu washtakiwa hao walipofikishwa
mahakamani.Katika kesi
hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 16 pamoja na vielelezo mbalimbali
huku washtakiwa hao wakijitetea wenyewe pasipo kuleta mashahidi wengine.
Washtakiwa hao
walikuwa wakitetewa na wakili wao, Hudson Ndusyepo, huku upande wa mashtaka
ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mwandamizi Prospar Mwangamila.Washtakiwa
wanadaiwa kati ya mwaka 2007 na Machi 2009 katika Makao Makuu ya DECI, Mabibo Dar es Salaam walikusanya
fedha kutoka kwa wananchi wakiwaahidi kuwa watapata faida ya riba kubwa. Mpango
huo uliitwa wa kupanda na kuvuna ambapo wanadaiwa kufanya shughuli hiyo bila
leseni.
Juni 12, 2009,
washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi Na.109 ya
kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria
ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.Kampuni ya DECI
iliyowanufaisha watu wengi hasa wale waliojiunga mwanzoni, iliibua malumbano
kati ya Serikali, viongozi wa kampuni hiyo na wanachama wao, waliopinga hatua
ya Serikali kusitisha shughuli zake kwa madai kuwa haiko kihalali.
Kusimamishwa
kwa shughuli za kampuni hiyo, kulitokana na uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
kutoa taarifa ya kutahadharisha Watanzania waliojiunga na upatu huo kuwa,
taasisi hiyo haiko kisheria na wanaweza kupoteza fedha zao walizopanda.Shughuli za
kupanda na kuvuna mbegu DECI zilisitishwa baada ya Serikali kusimamisha akaunti
za kampuni hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika, hali ambayo baadaye
ilisababisha uvunjifu wa amani katika ofisi za kampuni hiyo, baada ya wanachama
wake kuamua kuchukua sheria mkononi kwa kuvunja vioo vya magari ya viongozi,
wakitaka warejeshewe fedha zao.
Inadaiwa kuwa zaidi ya Watanzania
700,000 nchini walijiunga na taasisi hiyo na walikuwa wakipanda na kuvuna pesa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuchukua amana
za watu bila ya kibali kwa kuwa waliomba kibali cha kuendesha shughuli za
kifedha na si cha kuchukua amana ambapo katika utetezi wake Mchungaji Mtares
alikiri kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliwakataza kupokea fedha kutoka kwa
mwanachama yeyote wa taasisi hiyo .
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Prosper
Mwangamila, Mtares alidai katika barua ya majibu ya kuomba leseni ya kufanya
shughuli za taasisi hiyo, BoT iliwakataza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama
yeyote iwe kwa hiari au kwa lazima.
Hata hivyo alipoendelea kuhojiwa na
kupewa barua hiyo ambayo ilipokelewa mahakamani hapo kama
kielelezo cha upande wa mashtaka, Mtares alidai kuwa Mkurugenzi mwenzake ambaye
pia ni mshitakiwa ndiye atakayetoa maelezo zaidi.
Katika utetezi wake Mtares aliwasilisha
kielelezo ambacho ni barua ya maombi waliyoandika kwa Gavana wa Benki Kuu (BoT)
kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi ambazo ni kusaidia watu wenye
kipato cha chini kujikimu kimaisha.
Mtares aliendelea kudai kuwa, Benki ya
Afrika (BOA) ilikataa kuhifadhi fedha za taasisi hiyo hivyo walizihamishia
katika akaunti ya kanisa lake la Jesus Christ Deliverance iliyopo katika Benki
ya Wananchi Dar es Salaam (DCB) ambayo ilikutwa na zaidi ya sh. bilioni 1.3
baada ya shughuli za DECI kuzizuia.
Alipoulizwa sababu za benki hiyo
kukataa kuhifadhi fedha hizo, alidai hajui bali walipewa taarifa kuwa
wanatakiwa watoe fedha hizo haraka ndipo bodi ya wakurugenzi ilipoamua fedha
hizo ziwekwe kwenye akaunti ya kanisa lake.
Aliendelea kudai kuwa wanachama
walikuwa wanalipa kiingilio cha sh. 30,000 na baadaye wanaweka fedha na kupata
uwezeshwaji (riba) ya asilimia 150 ya fedha ambayo mwanachama ameweka.
Alipobanwa kwa maswali na upande wa
mashtaka, Mtares alidai fedha za riba zilitokana na fedha walizokuwa wanaweka
wanachama kwa sababu DECI ilikuwa haijishughulishi na biashara yeyote zaidi ya
kusaidia watu wenye kipato cha chini.
No comments:
Post a Comment