Na Thomas
Mtinge, Mbeya
MAKATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ngazi ya wilaya na mikoa nchini, wameagizwa kuwafukuza makatibu wa jumuiya za
chama hicho watakaohudhuria vikao vya Sekretarieti bila kuwa na ajenda za vikao
hivyo.
Agizo hilo
limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya CCM, Abdallah Bulembo,
wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM,
Mabaraza ya Wazazi,UWT na UVCCM katika wilaya za Mbalali na Kyela juzi.Kwa mujibu wa
Bulembo, kila mjumbe anayehudhuria vikao hivyo lazima awe na ajenda ya
kuiwasilisha katika kikao husika ili iweze kujadiliwa kwa pamoja na kuipatia
ufumbuzi.
"Vikao vya
Sekretarieti si vya kukutana kwa ajili ya kunywa soda na kupika majungu, bali
ni vikao vya kujadili mambo muhimu ya nchi na mustakabali wa chama,"
alisema na kuongeza;"Sasa kama
kuna wajumbe waonadhani hivyo ni vikao vya kunywa soda na kupika majungu, basi
wafukuzwe maana hawatufai wameshindwa kazi, hivyo mtoe nje ili akajipange tena
wala huna haja ya kumuonea aibu wala kufanya naye kazi kwa mazoea,"
alisema Bulembo.
Alisema pamoja
na mambo mengine, wajumbe hao wanatakiwa kujadili kero za wananchi na
kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu pale inapowezekana."Katika vikao vyenu mnatakiwa
kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafanikio ya utekelezaji wa Ilani
ya uchaguzi ya chama chetu na kero za wananchi," alisema.
Alisema baada ya kujadili ajenda hizo,
viongozi hao kwa pamoja wanatakiwa kushuka chini na kufanya mikutano ya hadhara
ya wananchi ili kuwaeleza mafanikio ya utekelezaji wa ilani hiyo na mikakati
iliyopo ya kutatua kero zao ili kuepuka upotoshaji unaoweza kufanywa na vyama
vya upinzani.
Bulembo alisema baadhi ya vyama hivyo
vya upinzani vimekuwa vikiwarubuni wananchi kwamba CCM haijafanya maendeleo
yoyote tangu kuingia kwake madarakani jambo ambalo alisema si kweli.
"Mwenye macho haambiwi tazama.
Hakuna mwananchi asiyejua au kuona mazuri mengi yaliyofanywa na serikali ya CCM
katika nchi hii. Wapinzani wanapita mitaani na kuwadanganya wananchi kwa
kuiponda Serikali ya CCM hao wamefilisika kisiasa kutokana na kuwa na mawazo
mgando kifikra.
Ili kuepuka propaganda hizo, nendeni
kwa wananchi mkakisemee chama chenu kwa kufanya mikutano ya hadhara na kuelezea
mafanikio yaliyofanywa, yaliyopo na yanayotarajiwa ili wawapuuze," alisema
Bulembo.
Alisema bila kufanya hivyo wananchi hao wanaweza kuamini kila
kitakachosemwa na wapinzani hao hata kama hakina ukweli.
No comments:
Post a Comment