22 July 2013

PINDA ANENA TOZO YA SIMU



Na Mwandishi Maalum, Ruvuma

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tozo iliyopitishwa na Bunge ya sh. 1,000 kwa matumizi ya simu za mikononi sio ya kuwaumiza wananchi, bali mapato yake yatakwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.Kwa mu j i b u wa t a a r i f a iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Pinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Songea ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya wiki moja katika Mkoa wa Ruvuma, baada ya kuutembelea Mkoa mpya wa Njombe."Toza hii ni kama ile iliyoongezwa kwenye mafuta ya petroli ambayo imetupa fedha nyingi kwenye mfuko wa ujenzi wa barabara (National Road Fund) za kuunganisha miji na mikoa na nyingi zimejengwa nazinaendelea kujengwa," alisema Waziri Pinda na kuhoji;"Nani asiyetaka vijiji vipate umeme kama miji, ili usaidie kuondoa giza, uendeshe viwanda vidogo vidogo na usaidie kukuza uchumi?. wanaopinga tozo hii, hawatutakii mema."Bunge la bajeti, lililomalizika mwezi uliopita, lilipitisha tozo ya sh. 1,000 kwa matumizi ya simu za mikononi ili fedha zitakazopatikana zisaidie katika mpango mkubwa wa kueneza umeme vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Umeme Vijijini, REA


.Kwa Mkoa wa Ruvuma peke yake, vijiji vipatavyo 150 vitapatiwa umeme chini ya mpango huo. Katika mikoa yote nchini kuna idadi inayotofautiana ya vijiji vingi vitakavyonufaika katika mpango mkubwa wa kueneza umeme vijijini ambao haujapata kutokea.Umeme umo katika sekta ya nishati ambayo ni moja ya sita zilizoteuliwa kutekelezwa chini ya mpango wa kuhakikisha matokeo makubwa yanapatikana sasa (Big Results Now) wenye upeo wa miaka mitatu, kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2013/14. Sekta nyingine ni Kilimo, Uchukuzi, Maji, Elimu na Mapato.

Kabla ya mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alizindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi, VETA, cha Songea kinachodahili zaidi ya wanafunzi 500 na pia kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa ufundi stadi mbalimbali.

Mapema Waziri Mkuu Pinda alisema bei ya mahindi kutoka kwa mkulima katika Mkoa wa Ruvuma, itakuwa ni sh. 500 kwa kilo badala ya sh. 450 ili wakulima wahamasike kuuza mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la kimataifa katika Kijiji cha Mkenda kwenye mpaka na Msumbiji, ikiwa ni moja ya masoko 48 yatakayojengwa mipakani kurahisisha biashara na kukabiliana na magendo.

1 comment:

  1. We Pinda Acha uhuni. Waone watu huko ulkotembelea na shida za maisha. Kusanya kodi za madini, Rudisha pesa za mafisadi, Wafungulie kesi wote viongozi wa CCM wanaopokea rushwa, na uwazibiti watu wako serikalini waibao kutumia kalamu.
    Ni mtoto wa Mkulima uliyefika Ulaya ukasahau ulikotoka na kuingia mjini. Huna mbele wala nyuma kwa sasa. Umeponea chupuchupu mara mbili, ondoka kaa kando na achia njia kwa wenye kisomo safi na ubavu wa kupigania haki.Kucheza ligwamba somngea ni kujiaibisha kwa hali ya juu. Kalee vijukuu, umeshatunisha mfuko wako. Unaaibisha Taifa kwa sasa na unajiaibisha Mwenyewe. Huna musuli.

    ReplyDelete