Na Lilian Justice, Morogoro
HALMASHAURI ya Wilaya
ya Kilombero imebainisha kuwa kuendelea kupata hati inayoridhisha katika
ukaguzi wa mahesabu yake ni kutokana na kuwepo ushirikiano mzuri baina ya
madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo.
Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkaguzi mkazi kutoka ofisi ya
ukaguzi Mkoa wa Morogoro, Jacob Ndaki wakati akisoma taarifa ya ukaguzi katika
halmashauri hiyo katika kikao cha baraza la madiwani ambapo alisema kuwa
halmashauri hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuonesha kwa vitendo juu ya
uwazi na uwajibikaji wa pamoja kwani kwa mfululizo wa miaka mitatu imekuwa
ikipata hati hiyo.
Ndaki alisema kuwa halmashauri hiyo inatakiwa kuendeleza juhudi
hizo na kusimamia ipasavyo mapato na matumizi katika vijiji na kata zake zote
ili utendaji kazi wake uweze kustawisha halmashauri hiyo, mkoa na Taifa kwa
ujumla.
Aidha alifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2011/2012 halmashauri
hiyo imeonesha kuimarika katika kufunga na uainishaji wa taarifa zake zenye
picha sahihi ya pato na matumizi na kuutaka uongozi kuelekeza nguvu katika
kuboresha zaidi huduma.
Alisema katika ukaguzi huo masuala mbalimbali yalipewa msisitizo
wa pekee katika taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali huku
akiainisha baadhi ya changamoto ikiwemo ya kutorejeshwa hazina mishahara
inayokadiriwa kufikia shilingi milioni 49.
Alisema nyingine ni asilimia 20 ya ruzuku ya vyanzo vilivyofutwa
kutopelekwa vijijini mfano kati ya shilingi milioni 88 ni shilingi milioni 55
zimebainika kupelekwa vijijini huku shilingi milioni 33 zikiwa hazijapelekwa.
Hata hivyo Mkaguzi huyo alisema kuwa katika manunuzi mbalimbali
shilingi milioni 22 zilihusika kati ya hizo kiasi cha shilingi milioni 14 ni
manunuzi yaliyofanywa kwa njia ya masurufu huku taarifa ikionesha kuhakikiwa
shilingi mil.4.6 wakati shilingi mil.17.8 zikionesha hesabu zisizoridhisha.
No comments:
Post a Comment