Na Mwajabu Kigaza, Kigoma
IMEBAINIKA kuwa
asilimia 97 ya wanawake wenye ugonjwa wa fistula huachwa na waume zao pamoja na
kunyanyapaliwa na jamii kutokana na kukutwa na tatizo hilo. Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa hospitali ya CCBRT ya Dar es
Salaam, Kaspar Mmuya wakati wa kikao maalumu kilichofanyika wilayani Kasulu kwa
lengo la kugawa rasilimali kati ya Wilaya mpya ya Buhigwe na Wilaya Kongwe ya
Kasulu mkoani Kigoma.
Mmuya alisema kuwa tatizo linalowakumba akinamama hao imekuwa
kikwazo katika familia zao na jamii kwa ujumla kuwatenga kutokana na tatizo hilo linalotokana na
uzazi. Aidha aliwataka viongozi wa kata,washirikiane na madiwani
kuelimisha jamii ili iondokane na tabia hiyo ya unyanyapaa kwa akinamama hao
pamoja na waume zao kushirikiana na akinamama hao kuwapatia matibabu.
Akitoa taarifa za utafiti uliofanywa na CCBRT kwa ushirikiano na
utawala wa Hospitali ya Kabanga, Dkt. Alphonce Lutumo alisema kuwa asilimia 97
ya wanawake wameachika toka kwa waume zao na asilimia 95 ya watoto wanaozaliwa
hupoteza maisha.
Dkt.Lutumo amesema kuwa, Januari 2013 hadi Julai wanawake sita
walifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Kabanga wilayani Kasulu mkoani Kigoma
ambapo hivi karibuni kutakuwa na kampeni ya fichua waathirika wa fistula
wilayani Kibondo.
Aidha Mganga mkuu msaidizi Hospitali ya Kasulu, Dkt. Cosmas
Buguzi aliipongeza Hospitali ya Kabanga kwa kushiriki vyema kwenye kampeni hiyo
ambayo inatoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi waliopo katika Wilaya za Buhigwe,Kakonko,Kasulu,
Kibondo, Kigoma na Uvinza mkoani Kigoma.
No comments:
Post a Comment