- ASEMA ATAKAYEJARIBU KUTUCHOKOZA ATAKIONA
- MWAMUNYANGE: TUPO TAYARI SIKU, SAA YOYOTE
Waandishi Wetu, Dar na Bukoba
AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama, Rais Jakaya Kikwete, amewahakikishia Watanzania kuwa vikosi vya
usalama nchini vipo tayari siku na saa yoyote, kuhakikisha amani inalindwa na
havitakubali kuona nchi inamegwa na mtu yeyote.
Rais Kikwete alitoa
kauli hiyo mkoani Kagera jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya
Mashujaa iliyofanyika katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
iliyopo Kaboya, wilayani Muleba.
"Hatutaruhusu
mtu yeyote achezee amani tuliyonayo wala kuruhusu mtu amege nchi yetu,"
alisema Rais Kikwete na kuongeza, "Kama
tuliweza kwa Idd Amin hakuna mtu yeyote atakayechezea nchi yetu," na
kuongeza;
"Wananchi laleni
usingizi msisikilize maneno na vitisho nchi iko imara atakayejaribu atakiona
cha mtemakuni."
Alisema jeshi lipo
macho wakati wowote na atakayethubutu kutuchezea atakiona cha mtemakuni.
Aliwataka wananchi wasiwe na wasiwasi wowote wala kuogopa vitisho kwani jeshi hilo lipo imara kulinda
usalama wa nchi.
Alisisitiza kuwa
kulinda nchi ni gharama kubwa, ndiyo maana wakati wa vita vya uvamizi wa Idd
Amin wapo waliopoteza maisha, kupata ulemavu, lakini hatupo tayari kupoteza
amani.
Kuhusu wanajeshi
wastaafu waliopata ulemavu wakati wa vita, Rais Kikwete, alisema Serikali
imekuwa ikiwahudumia na haitaacha kufanya hivyo, ingawa kuna manung'uniko
katika baadhi ya maeneo.
"Tunawakumbuka
na tutaendelea kuwahudumia kama kuna ambacho hakiendi vizuri niambieni ili
tukae na wenzetu wa jeshi kuondoa malalamiko kwa kudhamini gharama za maisha
yao waliojitoa muhanga kwa ajili ya nchi yetu," alisema Rais Kikwete na
kusisitiza kwamba Serikali haitaki wasikitike.
Aliwakumbusha Watanzania sababu za Jeshi la Tanzania kupigana vita na Uganda mwaka
1978. Alisema Amin hakuheshimu mipaka iliyoachwa na Wakoloni. "Amin aliona
Wakoloni wamekosea ramani kamili ya mpaka hivyo kuamini kuwa ni rahisi kwake
kuonesha ubabe kwa nchi yetu," alisema Rais Kikwete na kuongeza;
"Uongozi
uliokuwepo wakati huo chini ya Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu
Julius Nyerere) kila ulipomwambia aondoke alikataa na jawabu ilikuwa ni
kumuondoa kwa nguvu ili kukomboa nchi, mali na wananchi wake."
Alisema baada
ya kumuondoa nje tuliona ameacha amebomoa majengo yetu na kuharibu mali, hivyo na Tanzania
iliamua majeshi yake yaingie Uganda
yabomoe majengo ili nao wapate gharama za kujenga. "Hiyo ndiyo ilikuwa
maana ya Masaka na Mbalala," alisema na kuongeza;"Baada ya
kufika huko, tukaona tukimuacha ataendelea kuwa tatizo na usalama wa kudumu wa
nchi hautakuwepo maana hata kwa Waganda waliokuwa wakishangilia ushindi wa
majeshi yetu, Amin alianza kuwatisha kwamba watakiona baada ya majeshi ya Tanzania
kuondoka."
Alisema hapo ndipo ilipotolewa amri ya
saka joka popote lilipo likipatikana hata kwenye shimo likatwe shingo
vinginevyo likimbie na kazi ilifanyika na hapo ndipo mashujaa wetu wengine
walipoteza maisha na wengine kubaki na ulemavu.
Alisisitiza kuwa dhamira ya kulinda
nchi bado ipo na atakayejaribu kumega ardhi ya Tanzania atakiona.
Kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya
wanajeshi wa kambi ya Kaboya na wananchi, Rais Kikwete alimwagiza Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kukaa na jeshi na
viongozi wa vijiji ili kumaliza tatizo hilo.
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis
Mwamunyange, aliwahakikishia Watanzania kuwa jeshi lipo imara kuwalinda wakati
wote wa saa 24, hivyo wasiwasi uondoke na wananchi wafanye kazi za kuinua
uchumi.
Imeandikwa na Theonestina Juma,
Livinus Feruzi, Bukoba, Mariam Mziwanda na Anneth Kagenda, Dar
katika suala la ulinzi wa nchi na raia wake tuko pamoja,ingawaje mapungufu ni mengi sana mkuu.
ReplyDelete