Na Theonestina Juma, Kagera
ULEGEVU wa maofisa wa
Idara ya Uhamiaji nchini hasa maeneo ya mipakani umetajwa kuwa chanzo cha wahamiaji
haramu kufikia zaidi ya 56,000 kutokana na kujua bei zao ndogo, jambo ambalo ni
tishio na hatari kwa usalama wa nchi kwa miaka 50 ijayo. Kauli hiyo imetolewa na Rais Jakaya Kikwete, wakati wa majumuisho
ya ziara yake ya siku sita mkoani hapa.
Alisema ulegevu wa maofisa wa idara ya uhamiaji haramu ya kutokuwa
wafuatiliaji , wao ni chanzo na sehemu ya tatizo, kwani pindi watu hao
wanapoingia hakuna anayewafuatilia na kuwauliza wameingiaje nchini, kibali kiko
wapi, matokeo yake wanaingia nchini kwa kasi ya ajabu. Alisema maofisa hao wanatakiwa kusimamia kikamilifu utambuzi wa
watu wasio raia na kufuatilia vitabu walivyopeleka maeneo ya vijijini, kata na
tarafa.
"Kuna watu wanaishi nchi hii kwa kibali cha mtendaji wa
kijiji, ofisa mtendaji wa kata, kwa kuhongwa ng'ombe wawili, lakini kwa afisa
uhamiaji makini lazima amfuatilie yule mtu na kumuuliza umeingiaje humu,
akimwonesha kibali cha mtendaji awakamate na kuwapeleka wote mahakamani kwani
wanakuwa wameingilia kazi ya Idara ya Uhamiaji," alisema.
Alisema katika suala hili la wahamiaji haramu, msako sio jibu
akiingia nchini aondoke kwani Serikali haiwezi kupata sh. milioni 800 kwa ajili
ya kushughulikia tatizo hilo. Pia Rais Kikwete
alisema kuwa chanzo cha kuharibika kwa usalama kwa upande wa Kagera ni kutokana
na kuingia kwa wakimbizi nchini ambapo mwaka 1963 walikuwa ni wa aina nyingine
ambapo tena walioingia mwaka 1993 waliingia nchini na bunduki zao.
No comments:
Post a Comment