02 July 2013

HISTORIA

•Msafara wa Rais Obama magari 33, Dar yazizima

•Ulinzi wake washangaza wengi, barabara zafungwa

•Ammwagia sifa Rais Kikwete, kumaliza ziara yake leo


Mapokezi ya Rais Barack Obama wa Marekani alipowasili jijini Dar es Salaam jana. Rais Obama yuko katika ziara ya siku mbili nchini.



Na Waandishi Wetu

MAELFU ya wakazi wa Dar es Salaam, jana wamejitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Rais wa Marekani, Bw. Barack Obama ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku mbili, akitokea nchini Afrika Kusini ambako alifanya ziara ya siku mbili.

Katika ziara hiyo, Rais Obama ameongozana na mkewe Mama Michelle, watoto wao Maria (10), Sasha (7) na ujumbe wake.

Rais Obama aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, saa 8:30 na ndege yake aina ya Air Force One. Alipokelewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Baada ya ukaribisho huo, alikagua gwaride maalumu ambalo liliandaliwa kwa ajili yake, kupigiwa mizinga 21 na kuangalia ngoma za asili zilizokuwa zikitumbuiza uwanjani hapo.

Ngoma hizo zilimvutia Rais Obama ambaye alihamasika kuzicheza akionekana mwenye furaha.

Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa wa kwanza kuondoka uwanjani hapo kwenda Ikulu, baadaye kufuata Rais Obama ambaye alitumia gari maalumu aina ya Codillac One.

Msafara wa Rais Obama ambao ulikuwa na magari 33, uliondoka uwanjani hapo kwenda Ikulu, saa 9:15 alasiri. Baada ya kuwasili Ikulu, alifanya mazungumzo ya faragha na Rais Kikwete na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.

Rais Obama azungumza

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Rais Obama alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo muhimu na kusisitiza kuwa, Tanzania ina uwezo mkubwa wa kukuza uchumi wake.

“Ziara yangu imelenga kuboresha taasisi zilizopo nchini pamoja na kuchochea ushirikiano katika programu mbalimbali, nchi yangu ipo tayari kuisaidia Tanzania katika sekta ya nishati na umeme.

“Pia ziara yangu imelenga kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha biashara, kutokomeza ugonjwa wa malaria na vifo vya watoto...naipongeza Serikali ya Rais Kikwete kwa kusaidia kuimarisha usalama huko Darfur, Sudan,” alisema.

Rais Obama pia alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein na kusisitiza kuwa, Serikali ya Marekani itazidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya usalama kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho.

Alipoulizwa na mwandishi, Bw. Peter Ambikile juu ya Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeifanyia nini Tanzania, Rais Obama alisema nchi yake imesaidia kupunguza ugonjwa wa malaria na mpango huo umekuwa na mafanikio makubwa.

Aliongeza kuwa, Marekani pia inalenga kuiwezesha Afrika katika masuala ya umeme na kuiwezesha kuzalisha chakula cha kutosha.

Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema MCC imekuwa na msaada mkubwa kwa Tanzania ambapo malengo yaliyopo ni kuongeza usambazaji wa huduma na upatikanaji wake jijini Dar es Salaam pamoja na umeme vijijini.

Alisema Serikali ya Marekani imefanya mambo mengi kwa Tanzania kama kupunguza vifo vya watoto, maambukizo ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Katika ziara hiyo, Rais Obama alipata fursa ya kupanda mti ambao utabaki kuwa kumbukumbu kwa Tanzania.

Ulinzi mkali

Kuanzia asubuhi, maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam yalikuwa shwari ambapo askari wa Jeshi la Polisi wakiwa na magari, waliimarisha ulinzi wakiwa na silaha za moto pamoja na mbwa.

Katika uwanja wa ndege, makachero wa Marekani na Tanzania, walishirikiana kuweka ulinzi katika maeneo yote yanayozunguka uwanja huo na barabara zilizotumiwa na viongozi hao.

Mapokezi yake yatikisa

Mamia ya wananchi walikusanyika katika barabara aliyopita Rais Obama kwenda Ikulu wengi wao wakiacha shughuli zao na kutoka maofisini ili kuangalia msafara wa kiongozi huyo ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu.

Awali askari wa Vikosi vya Upelelezi vya Marekani (FBI), walijikuta katika wakati mgumu baada ya kushindwa kutambua barabara ambayo angepita Rais Obama akitokea uwanja wa ndege kutokana na ukosefu wa vibao vinavyoonesha majina ya barabara.

Akizungumza na gazeti hili, Ofisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema, kutokana na hali hiyo Serikali ililazimika kuweka vibao katika barabra ya Sokoine Drive na Gerezani.

Wanasiasa watoa maoni

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga, alisema ujio wa Rais Obama ni fursa nzuri kwa Tanzania katika kuimarisha demokrasia, uchumi na kuchochea uwekezaji endelevu katika sekta za nishati, miundombinu, viwanda, kilimo.

“Ziara ya kiongozi huyu ambaye ni rais wa 44 nchini Marekani, itasaidia kuhamasisha wawekezaji wajitokeze kwa wingi katika sekta mbalimbali nchini...hakuna cha ajabu kwa Taifa kubwa kama hili kushirikiana na Tanzania,” alisema Bw. Makamba.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema ujio wa kiongozi huyo unaweza kuwa na faida ya kukuza uchumi kama misaada inayotolewa na nchi hiyo itafanyiwa kazi kwa vitendo.

“Tunatambua jinsi Taifa hili linavyoisaidia Tanzania kupitia mipango mbalimbali ila nchi yetu inakabiliwa na tatizo la kushindwa kujipanga ili kufikia malengo... tunapaswa kuondokana na hali hii ili kukuza uchumi.

“Kimsingi ujio wa Rais Obama hauwezi kubadilisha maisha ya Mtanzania au jambo lolote, sisi tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na kujipanga kwa kutumia rasilimali tulizonazo,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), kilichopo mkoani Mwanza, Profesa Mwesiga Baregu, alisema ziara hiyo inaweza kuwa na faida kwa Tanzania kama wenyeji wake wamejipanga kumweleza mahitaji yao.

“Kwa mtazamo wangu naona Rais Obama amekaribishwa nchini hivyo ujio wake unaweza kuwa na faida kama waliomkaribisha watakuwa wamejipanga kwa hoja nzuri, Sitarajii kama tutawapa nafasi kubwa katika suala la usalama au nishati badala yake tuangalie mbali zaidi ili kuimarisha mambo yetu,” alisema.

Maoni ya wananchi

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam walioshiriki katika mapokezi hayo, walisema wamefurahishwa na ujio wa kiongozi huyo ambao ni neema kwa Tanzania hasa kwa kukuza uchumi wake.

Bw. Dadi Nahinga, alisema yeye binafsi amefurahi kumuona Rais Obama akiwa nchini kwani siku zote alikuwa akimuona katika televisheni akimfananisha na kiongozi shupavu mwenye msimamo na mapenzi makubwa kwa Tanzania.

Naye Bw. Heri Mahonyo, alisema alitegemea kumuona Rais Obama akiwa kwenye gari la wazi akiwapungia mikono wananchi ambao wamejitokeza kwa wingi kushuhudia msafara wake.

“Enzi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi anapokuja nchini alikuwa akitumia gari la wazi ili kupungia mikono watu waliojipanga barabarani tofauti na sasa,” alisema.

Kwa upande wake, Bw. Godfrey Ndyanabo alisema ujio wa Rais Obama una manufaa makubwa kwa Tanzania kwani anaamini mikataba ambayo ataisaini, italeta tija kwa Taifa.

Alisema Watanzania wanapaswa kuendeleza uzalendo wao kwani kitendo cha kujitokeza na kumlaki kiongozi huyo ni utamaduni tuliojengewa na waasisi wa Taifa hili.


Bw. Saidi Maganga, mkazi wa Kariakoo, alisema ziara hiyo ni fursa nzuri kwa Tanzania kujitangaza kimataifa na vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa mbalimbali
 nchini.
Mkazi mwingine, Bi. Irene Mkumbusho anayeishi Mbagala, alisema Rais Obama ameonesha mapenzi yake kwa Tanzania kwani nchi nyingi za Afrika zinamuhitaji hivyo anaamini ujio wake utachochea maendeleo ya sekta mbalimbali.
Alisema pamoja na ziara hiyo kuwa na manufaa kwa Tanzania, wakazi wa jiji hilo wamepata usumbufu mkubwa ambapo barabara nyingi zimefungwa hivyo wamelazimika kutembea kwa miguu.
Bw. Cyprian Basenga alisema, Serikali ikiamua inaweza kuboresha usafi wa mazingira kama ilivyofanya katika ziara ya Rais Obama hivyo aliomba utaratibu huo uendelee.
Alisema pamoja na ujio wa Rais Obama kusababisha usumbufu kwa wananchi, una faida kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na uwekezaji wake katika sekta ya umeme kupitia mradi mkubwa ambao utawanufaisha wananchi wengi.
Aliwataka wananchi kuachana na fikra potofu kuwa Rais Obama amekuja Tanzania kwa masilahi binafsi hivyo umefika wakati wa kuachana na mawazo hayo bali ugeni huo ni neema kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo ili kuuliza ugeni huo nchi yao inatumia njia gani kupandisha uchumi wao ili mbinu hizo ziweze kutumika nchini.
Bw. Iddy Fundi mkazi wa Mbagala, alisema ujio wa Rais Obama, umekwamisha shughuli nyingi za maendeleo ambapo wananchi wengi wametembea kwa miguu katika umbali mrefu
Alisema wafanyabiashara wengi wamelazimika kufunga biashara zao ili kupisha mapokezi ya kiongozi huyo na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi wa maeneo mbalimbali.
Kwa upande wao, wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo, walisema ziara ya kiongozi huyo imekwamisha biashara zao kutokana na wateja kushindwa kufika sokoni.
Walisema pamoja na hasara waliyoipata, wamefurahishwa na ujio wa Rais Obama ambaye amelifanya jiji hilo kuwa katika hali ya usafi na ulinzi kuimarishwa hivyo kupunguza vibaka ambao walikuwa kero kwa wateja wao na wananchi wengine.
“Kwa kweli mitaro ni misafi, hatukutegemea kama kuna siku ingeboreshwa na kuacha kutoa harufu...tunaomba mpango huu uendelee ili tuweze kujiepusha na maradhi,” walisema.
Wakati huo huo, mfanyabiashara wa nguo sokoni hapo, ameulalamikia uongozi wa jiji kwa kuwatuma askari wawanyang’anye bidhaa zao kwa sababu ya kufanya biashara kandokando ya Barabara ya Uhuru.
“Mimi naona ujio wa Obama hauna manufaa yoyote kwa sisi watu wa chini badala yake imetuongezea umaskini kwa kuchukuliwa bidhaa zetu ambazo zinatuingizia kipato cha kuhudumia familia, kulipia kodi ya nyumba na kufanyia mambo mengine,” alisema.
Bw. Alimas Issa, ambaye ni mfanyabiashara wa Bagamoyo, aliitupia lawama Serikali na kudai haijatoa elimu ya kutosha juu ya ujio wa kiongozi huyo.
Mwananchi apigwa
Saa chache kabla Rais Obama hajawasili nchini, mkazi wa Dar es Salaam ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alijikuta akipata kipigo kutoka kwa askari polisi katika eneo la Posta ya Zamani baada ya kumkashifu kiongozi huyo.
Baada ya kipigo hicho, kijana huyo alichukuliwa hadi Kituo cha Polisi Kati kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Watoto wazaliwa MNH
Jumla ya watoto tisa wamezaliwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), usiku wa kuamkia jana, siku ambayo Rais Obama na ujumbe wake aliwasili nchini.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Bw. Aminiel Algaesha, alisema kati ya watoto hao wanne wa kike na watano wa kiume.
Alisema watoto hao pamoja na mama zao wanaendelea vizuri ambapo hadi jana mchana wameruhusiwa kurudi majumbani.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wamelalamikia mwendo kasi wa msafara wa Rais Obama hivyo kukosa fursa ya kumuona.
Wananchi hao waliokuwa wamejipanga barabarani na kuongeza kuwa, kiu yao ilikuwa kumuona kiongozi huyo lakini ndoto hiyo imekuwa tofauti na walivyotarajia.
Bw. Hassan Hamza, mkazi wa Kivukoni, alisema amesimama barabarani tangu saa nne asubuhi lakini alishindwa kumuona kiongozi huyo kutokana na mwendo kasi wa msafara wake.
“Mimi nilijua angepita katika gari la wazi akitupungia mikono badala yake tukashuhudia mabenzi yake myeusi yakipita kwa kasi, hata kama kilichozuia ni sababu za kiusalama...bado angeweza kutupungia mikono,” alisema.
Aliongeza kuwa, “Si kweli kwamba tuliokaa barabarani hatuna kazi za kufanya bali ni utashi wetu tukitaka kumuona kiongozi huyu ndiyo uliotufanya tukae muda mrefu barabarani”.
Katika hatua nyingine, baadhi wa wananchi walionekana wakitoka katika ofisi zao na kujipanga kwenye Barabara ya Sokoine ili kushuhudia msafara wa kiongozi huyo.
Maofisa usalama waliokuwa katika barabara hiyo, waliimarisha ulinzi kwenye eneo hilo wengine wakiwaondoa watu waliosimama katika milango, madirisha ya ofisi zao ili wajipange barabarani.
Ziara ya Rais Obama imelenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi za Afrika. Kiongozi huyo pia ametembelea Senegal ambapo ujio wake Tanzania, ndiyo unahitimisha ziara yake barani Afrika.
Jana usiku Rais Obama aliandaliwa dhifa ya kitaifa na mwenyeji wake Rais Kikwete ambapo leo, atatembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Symbion iliyopo, Ubungo na kuhitimisha ziara yake ya siku mbili saa sita mchana katika uwanja wa ndege.




 

No comments:

Post a Comment