25 July 2013

FILAMU YA KKIZA, YANGA YAENDELEA Na Elizabeth Mayemba
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Hamis Kiiza ambaye amekuwa akiidengulia klabu hiyo kuongeza mkataba mpya jana jioni alitarajiwa kutua nchini akitokea kwao Uganda kwa ajili ya kuja kumalizana na klabu hiyo.
Awali Kiiza alikuja nchini kwa lengo la kumalizana na uongozi huo, lakini inadaiwa kuwa ilishindikana na hivyo akarejea tena Uganda.

Hata hivyo uongozi wa klabu hiyo, ulisema usingeweza kuzungumza lolote kuhusiana na mchezaji huyo mpaka pale mtu wake wa karibu ambaye ndiye aliyemleta, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, Mussa Katabalo aliyekuwa Ulaya kikazi, arejee na yeye ndiye atakuwa mtu wa mwisho na hatima ya mchezaji huyo itajulikana.
Akizungumza na gazeti hili jana mmoja wa marafiki zake wa karibu na Kiiza, alisema baada ya Katabalo kutua nchini mchezaji huyo jana alitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jioni akitokea kwao Uganda.
"Jamaa anakuja kumalizana na Yanga kwani, Katabalo ameshatua nchini mapema wiki hii, hivyo atazungumza na Kiiza na hatima yake itajulikana kama ataendelea kuichezea timu hiyo au la," alisema.
Rafiki huyo wa karibu na Kiiza alisema, mchezaji huyo anaipenda Yanga lakini kikubwa anachotaka ni kukamilishiwa matakwa yake, ili aweze kuitumikia klabu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.
Kiiza alimaliza mkataba wake na Yanga, hivyo akataka aboreshewe mshahara pamoja na fedha za usajili, lakini klabu hiyo ya Jangwani ikasema kuwa haiwezi kumlipa kiasi hicho cha fedha.
Mshambuliaji huyo alisema uwezo wake bado ni mkubwa, hivyo anashangaa ni kwanini uongozi wake unashindwa kufanya vile anavyotaka yeye kwa kuwa bado ana mapenzi mema na klabu hiyo.
Endapo Yanga itamsajili Kiiza anaweza kuigharimu zaidi ya sh. milioni 100, ambapo alitaka dola za Marekani 45,000 za usajili, nyumba ya sh.milioni 8.
Pia alitaka gari la sh. milioni 10 pamoja na dola za Marekani 3,500 kwa ajili ya mshahara wake kila mwezi. Lakini baadaye akatoa punguzo katika fedha za usajili na kutaka alipwe dola za Marekani 40,000.

No comments:

Post a Comment