Na Jovither Kaijage,
Ukerewe
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ukerewe Mwanza
inakamilisha mchakato wa sheria ndogo ya usafi wa mazingira ili kukabiliana na
tatizo hilo.Ofisa afya na
mazingira wa halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Bulugu amesema hayo baada
kushiriki shughuli ya usafi wa mazingira ambayo Jumatano ya wiki hii imefanyika
katika mtaa wa Mdoe mjini Nansio.
Akizungumza na wakazi
wa mtaa huo alisema mbali ya faini ya papo kwa papo ya sh. 10,000 pia sheria
hiyo inahusisha mambo mengine ikiwemo tozo ya sh. 4,800 kwa mwaka kwa kila
kaya.Adhabu ya sh. 10,000
itatozwa kwa mtu yeyote atakayetupa uchafu wa aina yoyote ovyo huku sheria ya
tozo za gharama za huduma zikitofautiana kutoka kaya hadi taasisi na miradi
binafsi ya biashara kama vituo binafsi vya
afya na shule, baa, nyumba za kulala wageni na maduka.
Sheria hiyo
inayotarajiwa kuwasilishwa katika baraza lijalo la madiwani inaonesha viwango
vya tozo kwa mwaka vitakuwa kati ya sh. 4,800 hadi 100,000 fedha ambayo
zikikusanywa zitatumika kuendesha gharama za usafi wa mazingira katika mji wa
Nansio.
Hata hivyo Bulugu
alisema sheria hiyo baada ya kupitishwa na baraza la madiwani itapelekwa kwa
waziri mwenye dhamana kabla ya kurejeshwa ili itumike kusimamia usafi wa
mazingira katika wilaya hiyo.
Awali ilipendekezwa
katika sheria hiyo itozwe adhabu ya papo hapo ya sh. 50,000 kwa anayetupa
uchafu ovyo kabla ya Mkuu wa wilaya hiyo, Mery Tesha kushauri kiwango hicho
kipunguzwe hadi sh. 10,000 ili sheria hiyo itekelezwe kwa urahisi
Tesha alisema kulingana na hali ya kipato cha wananchi walio wengi ni
duni hivyo kama faini itakuwa kubwa
haitatekelezeka na kusababisha walio wengi kushtakiwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment