29 July 2013

DAWA BANDIA ZAZAGAA MITAANI




 Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WAFUGAJI wa kuku katika Manispaa ya Shinyanga wametahadharishwa kutotumia chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa kideri baada ya kubainika kuzagaa kwa dawa bandia madukani.Tahadhari hiyo ilitolewa na Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Veran Mwaluko alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya kuzagaa kwa dawa hizo bandia ambapo alisema wafugaji watakaoendelea kutumia chanjo hiyo wanaweza kujikuta wakipata hasara kwa kuku wao kufa.

Dkt. Mwaluko alisema hapo awali Serikali ndiyo iliyokuwa ikizalisha na kusambaza dawa hizo kwa wafugaji lakini hata hivyo ilisitisha matumizi yake tangu Aprili mwaka huu na kwamba dawa zinazouzwa hivi sasa si dawa halisi.Kutokana na hali hiyo, ofisa mifugo huyo amewaomba wafugaji wote wa kuku katika manispaa ya Shinyanga kutoa taarifa katika ofisi yake au kituo chochote cha polisi pale watakapobaini kuwepo kwa watu wanaoendelea kuuza dawa hiyo bandia iwe dukani au wanaotembeza mitaani.  
Alisema utafiti uliofanywa na Serikali umebaini dawa hiyo haina uwezo wa kuzuia ugonjwa wa kideri na badala yake itawaathiri kuku hali ambayo itasababisha wafugaji wapoteze kuku wao ambapo amewashauri hivi sasa watumie dawa ya chanjo ya vidonge hadi serikali itakapotoa maelezo zaidi kuhusiana na chanjo hiyo ya matone.
 Hata hivyo Dkt. Mwaluko alisema tayari ofisi yake ilifanya msako ulioendeshwa na kitengo cha chanjo ya mifugo kanda ya ziwa (VIC) kilichopo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambapo chupa 1,000 za chanjo bandia zilikamatwa kutoka katika maduka mbalimbali yanayouza dawa za mifugo manispaa ya Shinyanga. Ma n i s p a a y a S h i n y a n g a inakadiriwa kuwa na idadi ya kuku wapatao 75,431 ambao ni wa kienyeji na wale wa kisasa wapo 14,393 kwa mujibu wa sensa ya mifugo iliyofanyika hivi karibuni katika manispaa hiyo.

No comments:

Post a Comment