16 July 2013

AIRTEL KUZINUFAISHA SEKONDARI 100



 Na Mwandishi Wetu
SHULE 100 za sekondari zitanufaika na mradi, Airtel Shule Yetu utakaowawezesha kupata vitabu vya kiada vitakavyowasaidia katika masomo ili kuongeza ufaulu.
Kampuni ya Airtel inayotoa huduma za mawasiliano katika nchi 20 barani Afrika na Asia, itatumia sh. milioni 150 katika mradi wa Airtel Shule Yetu pamoja na shule 100 zitakazofaidika katika msomo na kuongeza kiwango cha ufaulu nchini

Akizungumza jana Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando alisema, kwa miaka 11 mfululizo sasa Airtel chini ya mradi wa ‘Shule Yetu’ wameweza kuchangia katika sekta ya elimu na kuzifikia shule zaidi ya 950 na kutoa vitabu vyenye zaidi ya thamani ya sh.bilioni 1.6 mpaka sasa.
Alisema kuwa katika droo maalum iliyoendeshwa na Airtel hivi karibuni shule 100 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini zimechaguliwa na kuingia katika mradi wa shule yetu kwa mwaka wa 2013 - 2014.
“Tunafahamu jitihada za Serikali chini ya Wizara ya Elimu katika kupambana na changamoto hizi hivyo tunaungana na serikali katika kuinua sekta ya elimu kupitia mradi huu wa shule yetu ambao umeleta tija na kuleta mfanikio katika shule walizoweza kuzifikia.
Tunaahidi kuendelea kuisaidi jamii kupitia miradi yetu mbalimbali tuliyonayo hususan katika elimu,” alisema.
Awali Kaimu Mkurugenzi ukuzaji na rasilimali wa Mamlaka ya Elimu (TEA), Bi. Sylivia Gunze alisema kuna changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo uhaba wa vitabu shuleni ambapo kwa sasa uwiano wa vitabu shuleni ni kitabu kimoja kinatumika na wanafunzi 5 hivyo msaada huu utasaidia sana kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika shule zinazofaidika nchini.

No comments:

Post a Comment