JAMII ya
wafugaji mkoani Pwani wameshauriwa kujiunga na Mtandao wa Wafugaji Mkoa wa
Pwani (IPASO) kwa lengo la kuongeza umoja utakaowawezesha kufanikisha mambo
mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo sekta ya elimu, anaripoti Omary Mngindo,
Bagamoyo.
Rai hiyo
imetolewa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Bi.Keyana Kimunyu kwenye
mkutano ulioandaliwa na umoja huo na kuhudhuriwa na wafugaji zaidi ya 100
uliokuwa chini ya mwenyekiti wake, Bw.Letoni Leboi.
Bi.Kimunyu
alisema kuwa jamii ya wafugaji pamoja na kuwa na nafasi nzuri kiuchumi kutokana
na wengi wao kumiliki mifugo, lakini cha kushangaza hawatambui umuhimu wa elimu
hivyo kushindwa na jamii ya wakulima ambao wanategemea kilimo kusomeshea watoto
wao.
Alieleza kuwa
kwenye chuo kikuu anachosoma mkoani Dodoma, wanafunzi jamii ya wafugaji
hawazidi 15 na kuwa katika mahafari yaliyopita ni mwanafunzi mmoja tu wa
kifugaji aliyehitimu elimu chuoni hapo hali inayothibitisha kuwepo kwa upeo
mdogo kwa jamii hiyo kwenye sekta hiyo ya elimu.
Mwanafunzi
mwingine aliyethibitisha kauli ni Bi. Neema Mahungu ambaye alielezea masikitiko
yake kutokana na yeye kufanya vizuri katika elimu yake kidato cha sita lakini
mzazi wake ameshindwa kumwendeleza kielimu huku akimtaka mwanafunzi huyo
aolewe.
“Cha kushangaza
pamoja na kufanya vizuri katika masomo yangu katika shule ya Eaboishu iliyoko
jijini Arusha, mzazi wangu amenieleza hana uwezo wa kuniendeleza zaidi kielimu
huku akinitaka niolewe na tayari ameshanitafutia mchumba,” alisema mwanafunzi
huyo.
Kwa upande wake
Bw.Sheder Mkole alikuwa wa kwanza kutoa ushauri wa kuanza kuendeshwa kwa
harambee kabla ya kuendelea na mkutano huo ulioitishwa na umoja huo wa wafugaji
mkoani Pwani kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
Mratibu wa Umoja
huo Bw. Lekope Laini amewaeleza wana-IPASO hao kwamba lengo kubwa la umoja huo
ni kuhakikisha jamii ya wafugaji wanakabiliana na changamoto mbalimbali
zinazowakabili.
Katika harambee hiyo
zimekusanywa kiasi cha sh. 720,000 ambapo kati ya hizo sh. 130,000 ni taslimu
huku ahadi zikiwa sh. 570,000.
No comments:
Post a Comment