31 May 2013

Wenje, CUF ngoma nzito


*HOTUBA YAKE YALETA UTATA KWA WABUNGE CUF
*AKATAA KUOMBA RADHI, ASEMA KADHALILISHWA
*KAMATI KUMJADILI, NDUGAI AAHIRISHA BUNGE
Na Waandishi Wetu


 KWA mara nyingine, Naibu Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai, jana amelazimika kuahirisha kikao baada ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), kupinga baadhi ya maneno yaliyopo katika hotuba ya Kambi ya Upinzani.
Hotuba hiyo ilisomwa bungeni mjini Dodoma na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Ezekiel Wenje, ambaye ni Mbunge wa Nyamagana, Mwanza.
Wakati Bw. Wenje akiendelea kusoma hotuba hiyo, mbunge wa Jimbo la Mtambile, Bw. Masoud Salim (CUF), Zanzibar, alisimama na kuomba mwongozo wa spika na kutaka hotuba hiyo isitishwe akidai imejaa uzushi, uwongo na ushenzi.
Katika hotuba yake, Bw. Wenje alisema Chama cha CUF itikadi zake ni
za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji pamoja na ushoga.
“Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wa umoja wa Maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa nchini Uingereza, Lynn Featherstone, kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho kikipitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu,” alisema.
Katika mwongozo wake, Bw. Salim alitumia kanuni ya 68 (1) (a) inayosema, bila kuathiri masharti ya ibara ya 100 ya katiba inayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, mbunge hatatoa taarifa ambazo si za kweli, hatatumia lugha ya matusi na inayodhalilisha wengine.
“Natoa hoja kwamba, hotuba hii ni ya kizushi...huu ni uhuni, uwongo, ushenzi na uzandiki, hotuba hii si ya kusomwa bungeni,” alisema Bw. Salim akinukuu maneno yaliyopo kwenye hotuba ya Bw. Wenje.
Bw. Salim alikitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiombe radhi kutokana na kauli hiyo akiiomba Kamati ya Maadili ya Bunge iifanyie kazi kauli yao.
Kutokana na maelezo hayo, Bw. Ndugai alimuuliza Bw. Wenje kama
 na kumjibu kuwa;
“With due respect, ningeomba wabunge wenzangu wanisikilize kwa n z a . . . h a p a t ume e l e z a CHADEMA, CCM pamoja na CUF, juu ya uhusiano wao na mataifa ya nje.
“Ni ukweli kwamba CCM wako mrengo wa kushoto, CHADEMA mrengo wa Kati na CUF mrengo wa Kiliberali,” alisema Bw. Wenje, ambaye baada ya kutoa majibu hayo, wabunge wa CUF walisimama, kushika kitabu cha hotuba na kumfuata Bw. Wenje mbele ya Bunge.
Hali hiyo ilisababisha utulivu kutoweka bungeni ambapo Bw. Ndugai alilazimika kuahirisha Bunge hadi jioni na kuitaka Kamati ya Maadili ya Bunge, ikutane kwenye kikao cha dharura ili kuipitia hotuba hiyo.
Baada ya Bunge kuahirishwa, Bw. Wenje alitoka haraka akikimbia huku akisindikizwa na polisi hadi nje ya ukumbi wa Bunge ambako kulitokea zogo kubwa kati ya wabunge wa CHADEMA na CUF, kila upande ukitupiana maneno na vijembe vya hapa na pale.
Wabunge wa CUF walitishia kuwapiga wabunge wa CHADEMA, kama wataendelea na msimamo huo.
“Lazima waombe radhi na waache kuzushia chama chetu mambo ya uongo na kihuni,” alisikika akisema mbunge wa CUF ambapo wabunge wa CHADEMA, walisisitiza hawatafuta kauli yao kwa sababu wana uhakika na mambo waliyoyasema.
Kikao cha jioni
Kikao cha jioni kilianza kwa Bw. Ndugai kumpa nafasi Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Bunge, Bw. John Chiligati, aeleze uamuzi uliofikiwa na kamati yake kuhusiana na sakati hilo.
Bw. Chiligati aliliambia Bunge kuwa, kamati yake ilikutana na Bw. Wenje ambaye ni mlalamikiwa na Bw. Salim (mlalamikaji), ambapo walimtaka Bw. Wenje afute kauli zake kwa maandishi, aombe radhi na kamati itoe adhabu.
Hata hivyo, Bw. Wenje aligoma kuomba msamaha akidai hakukosea bali katika hotuba yake alieleza itikadi ya vyama vya mrengo wa Kiliberali na hakulenga chama chochote.
Pia Bw. Chiligati alisema, Bw. Wenje alikubali kuondoa maneno hayo kwenye hotuba yake, lakini hotuba hiyo iliporudi haikutofautiana na ile ya kwanza bali kilichobadilika ni maneno kuwa ya Kiingereza ambayo ni ya usagaji na ndoa za jinsia moja.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Bw. Ndugai alimpa dakika tano Bw. Wenje atumie fursa hiyo kufanyia kazi ushauri wa kamati iliyomtaka aombe radhi na kuondoa maneno hayo kwenye hotuba yake, lakini alikataa na kuhoji aombe msamaha kwa kosa lipi?
Alisisitiza kuwa, hawezi kufuta maneno ya ukweli na kudai hata yeye alitukanwa na kudhalilisha asubuhi kiasi cha kushindwa kumaliza hotuba yake.
Baadaye Bw. Ndugai alimpa nafasi mlalamikaji Bw. Salim ambaye naye alisisitiza kuwa, msimamo wake uko pale pale; hivyo ni vyema Bw. Wenje aombe radhi, kuondoa maneno hayo kwa maandishi na kamati ichukue hatua, vinginevyo hotuba isisomwe na CUF itamuunga mkono.
 Akitoa uamuzi wa kiti, Bw. Ndugai alimtaka Bw. Wenje aombe radhi na akubali kuondoa maneno yote yaliyokuwa yakikataliwa ili aweze kuendelea na hotuba yake.
Bw. Wenje aliinuka na kukubali kuondoa maneno hayo na kutaka kuendelea na hotuba yake bila kuomba radhi ambapo Bw. Ndugai alimkatisha kwa kumtaka akae chini na kutangaza kuahirisha kikao cha Bunge hadi leo asubuhi.
Alisema suala hilo linarudishwa tena kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kwa ajili ya maamuzi zaidi.
Habari hi i imeandikwa na Gladness Theonest, Kassim Mahege na Rachel Balama.

1 comment:

  1. Hawa jamaa wa chadema hawana ustaarabu kabisa, wanataka kugombana na kila mtu, kuwa rafiki na mwizi sio lazima na wewd uwe mwizi. Na hizi bajeti mbadala mbona zimejaa maneno ya udhalilishaji tu sio ikisomwa bajeti, au hawana wachumi wa kutengeneza wapo kina lisu tu watu wa maneno. Hawa ndo wanakiwa kupewa nchi hawa. Kweli upepo wa 2010 ulikuwa mbaya kabisa

    ReplyDelete