31 May 2013

Uandishi umechangia mateso ya Kibanda-Kamati


Mashaka Mhando na Rachel
Balama


 TUKIO la kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), ambaye anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini, limechangiwa na kazi yake ya uandishi wa habari likihusisha vyombo vya dola na vyama vya siasa.
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya uchunguzi wa tukio hilo, Bw. Deodatus Balile, aliyasema hayo mjini Tanga jana wakati akiwasilisha ripoti ya uchunguzi uliofanywa na watu watano.
Alisema kamati hiyo imebaini halina uhusiano wowote na masuala ya rushwa au mapenzi bali ni mpango maalumu ambao uliandaliwa na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasio waaminifu ili kutekeleza matakwa ya kisiasa.
“Kamati imebaini kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa katika kuandaa mpango wa kuteswa kwa Bw. Kibanda hatua ambayo uchunguzi huo umebaini kuwepo kwa sababu ya kutokea tukio hili,” alisema Bw. Balile.
Katika taarifa hiyo yenye kurasa 10 ambayo aliwasilishwa kwenye
Mkutano wa pili wa mwaka wa mashautiano kati ya Baraza la Habari nchini (MCT) na TEF,Bw. Balile alisema uchunguzi huo ulijikita katika mazingira ya tukio hilo kabla na baada ya kutokea.
Pia uchunguzi huo uliangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), na kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua.
Kamati hiyo ambayo ilitoa wito kwa Serikali kufuatilia kwa karibu na kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ili kupata ukweli na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wote waliohusika kumtesa Bw. Kibanda.
I l i p e n d e k e z a k u f a n y i k e marekebisho makubwa ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba vya habari ili kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.
Usalama wa wanahabari upewe kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla pamoja na kuwepo mafunzo ambayo yatawawezesha wanahabari kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.
Ripoti hiyo ilizitaka taasisi za habari zifanye juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), haraka iwezekanavyo ili kuzungumzia viashiria vya hatari vinavyoelekea kuvuruga amani ya nchi.
Bw. Kibanda aliumizwa kichwani na kusababisha baadhi ya mifupa yake kuvunjika, kutobolewa jicho lake la kushoto, kung’olewa meno na kucha bila ganzi na kumkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondoka nayo.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Bw. Rashid Kejo (Katibu), Pili Mtambalike, Jane Mihanji na Tumaini Mwailenge,

No comments:

Post a Comment