31 May 2013

Waziri ataja mbinu za kumaliza migogoro


Na Mwa j uma J uma ,
Zanzibar


 WAZIRI wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakar, amesema kuwa katika kutafuta amani na utulivu ni lazima pawepo na msimamo wa pamoja ili kuweza kufanikiwa kumaliza tofauti.
Waziri huyo aliyaeleza hayo katika uzinduzi wa kitabu cha Mizozo na namna ya kuitambua na kuitatua kisha kuichambua mizozo ya Zanzibar hafla iliyofanyika mjini Unguja.
Alisema kuwa katika kufikisha suala hilo pamoja na kuwepo na msimamo lakini hekima na busara itumike ili kufikia lengo la kupatikana kwake.
Hata hivyo alisema kuwa si njia sahihi ya kufikiria kuwa njia pekee ya kumaliza tofauti baina ya pande mbili ni kumshinda unaepambana nae bali ni kumshawishi ili akubaliane na mtazamo pamoja na unayoyasema.
Aidha, alisema kuwa kwa vyovyote vile kiini cha migogoro huwa ni
namna ya kutotendewa haki waonavyo upande mmoja au mabishano ya kidini, kutotimiziwa kwa matakwa yao muhimu ya kimaendeleo pamoja na suala zima la kudhibiti hali ya uchaguzi katika nchi husika.
Alisema kuwa mizozo ya aina hiyo huchukua aina ya ugomvi wa kiraia na kuanza kutengana baina ya kundi fulani na lingine ndani ya jamii, ambayo ndio yanayoifanya dunia kutafuta njia za usuluhishi baina ya watu hao wanaoishi ndani ya nchi moja.
"Zanzibar nayo haijakuwa nje ya matatizo hayo, ndio tukapata misukosuko mingi tu katika visiwa vyetu kuanzia mwaka 1995," alisema.
Mapema mjumbe wa Kamati ya Amani na Utulivu, Mchungaji Lusungu Leonard Mbilinyi alisema kuwa amani ndio nguzo ya kuleta maendeleo ya taifa lolote duniani, hivyo alisema kuwa Wazanzibari hawana budi ya kuungana na kutatua migogoro yanayojitokeza katika jamii yao iliyowazunguuka.

No comments:

Post a Comment