WAKAZI wawili katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi,wamefikishwa
mahakamani wakikabiliwa na shtaka la kujihusisha na masuala ya ujambazi kwa
kutumia silaha mbalimbali ikiwemo bunduki ya kienyeji na kufanikiwa kupora
bidhaa na fedha taslimu jumla ya sh milioni 1.2.
Washtakiwa hao
ambao kesi yao ipo kwa Hakimu Aluu Nzowa wa Mahakama ya wilaya hiyo ni, Hamisi
Athumani Mbuhi na Rajabu Juma Ndete wote ni wakazi wa mtaa wa Kongo mjini Lindi
na wamelazwa hospitali ya mkoa huo Sokoine.
Akiwasomea shtaka lao katika wodi namba sita walikokuwa wamelazwa
Mwanasheria wa
Serikali, Juma Maige alidai Mei 20 mwaka
huu usiku washtakiwa wote kwa pamoja walifika dukani kwa Hamisi Hassani Bakari
lililopo Kijiji cha Mkwajuni Wilaya ya Lindi na
kupora bidhaa na fedha taslimu.
Maige aliiambia
mahakama hiyo kwamba siku hiyo washtakiwa wakiwa na bunduki moja aina ya Shotgun
iliyofutwa namba zake pamoja na panga walifanikiwa kupora simu sita za
mkononi za watu waliozipeleka kwa ajili ya kuchaji na fedha taslimu
Sh.900,000/-na kufanya jumla ya sh.milioni 1.2.
Alidai mahakamani hapo kwamba siku hiyo washtakiwa wakiwa na silaha hizo
walifika dukani kwa mlalamikaji huyo na kuanza kupiga risasi hewani ikiwa na
lengo la kutisha majirani wasitoke nje nyumba zao kisha kuvunja mlango
wa duka lake na kupora bidhaa na fedha hizo na kutoka
nazo nje ambapo waliendelea kupiga risasi hewani hadi kuishiwa.
Mwanasheria huyo wa Serikali alidai
kwamba washtakiwa wamefanya kosa chini ya kifungu cha 287 kanuni ya adhabu sura
ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Pia aliiambia mahakama hiyo kwamba
kitendo cha watuhumiwa hao kuishiwa risasi kwenye bunduki yao kulitoa mwanya
kwa wananchi ambao walijitokeza na kufanikiwa kuwatia mikononi na kuanza
kuwapiga hadi kuishiwa nguvu.
Alidai kitendo cha kuishiwa nguvu
kuliwafanya wananchi hao kuendelea kujichukulia sheria mikononi ikiwemo
kuwafunika nyasi na kuwachoma moto kabla ya kuokolewa na Polisi waliofika
kijijini hapo muda mfupi.
Washtakiwa
wote kwa pamoja wamekana shtaka lao na kesi yao,namba 49/2013,imepangwa
kusikilizwa tena mahakamani hapo Juni 06 mwaka huu na wote wapo chini ya
uangalizi wa askari magereza katika hospitali ya Sokoine.
No comments:
Post a Comment