16 May 2013

Wauguzi walia kucheleweshewa mishahara

Na Steven William, Muheza



 WAUGUZI wa Afya katika Hospitali Teule wilayani Muheza wamedai kwamba wamekuwa wakicheleweshewa mishahara yao katika hospitali hiyo hali ambayo inasababisha wafanye kazi katika mazingira magumu.
Hayo yalisemwa katika risala ya wauguzi katika siku ya wauguzi duniani iliyoadhimishwa kiwilaya hivi karibuni katika Kijiji cha Magoda ambayo ilisomwa na Furaha Kiswaka.
Alisema kuwa wafanyakazi wa hospitali wamekuwa wakicheleweshewa mishahara hali ambayo inawafanya washindwe kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Kiswaka alisema pia wauguzi hao wanakabiliwa na tatizo la
nyumba kwa wanaoishi vijijini ambapo wanaishi katika makazi duni.
Alisema kuwa wauguzi wengine wanaishi mbali na vituo vya kufanyia kazi kitu ambacho wanahatarisha maisha yao hasa wakati wa usiku wanapokuwa na zamu huku wakishauri panapojengwa zahanati pajengwe na nyumba ya muuguzi.
Kiswaka alisema kuwa wauguzi wanakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba, vifaa vya usafi na mahitaji muhimu kwa ajili ya usafi ambapo alisema mganga mkuu wa wilaya amekuwa akijitahidi kupatikana vifaa hivyo isipokuwa hospitali ya wilaya Teule bado kuna uhaba mkubwa wa dawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muheza, Ibrahim Matovu ambae aliwakilishwa na Kaimu wake, Maurd Mbugi aliwataka wauguzi kufanya kazi kwa moyo mmoja ili kuboresha afya za wananchi na hatimae kuongeza uchumi wa nchi.
Alisema kuwa matatizo yote waliyoyaeleza ameyasikia na atayafanyia kazi kwa kuyapeleka kunakohusika ili yafanyiwe kazi na kuwataka wasife moyo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Zahanati ya Magoda, Leticia Ibrahim alisema kuwa zahanati hiyo wanatibu zaidi ya wagonjwa 20 kwa siku pamoja na kutoa huduma ya CHF.
Nae Muuguzi Mkuu, Victoria Wasapa aliongoza kuwaapisha wauguzi katika sherehe hiyo ili wawe na nidhamu katika kazi.

No comments:

Post a Comment