16 May 2013

Mwenge kumulika miradi ya zaidi ya bilioni 1/-

Na Steven William, Muheza


 ZAIDI ya miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 itapitiwa na Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga
Miongoni mwa miradi hiyo itakaguliwa, kufunguliwa na kuweka mawe ya msingi pindi utakapowasili wilayani humo Mei 18, mwaka huu.
Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na ujio wa Mwenge huo wa Uhuru wilayani humo.
Alisema kuwa miradi ambayo itapitiwa na Mwenge huo ni
pamoja na kukagua mradi wa hifadhi ya bahari Kijiji cha Kigombe, kufungua ujenzi wa nyumba ya mwalimu shule ya msingi Kijiji cha Mtiti.
Miradi mingine itakayotembelewa na Mwenge huo ni kukagua shamba la miti katika Kijiji cha Kigombe na kuweka jiwe la msingi Zahanati ya Kijiji cha Kilulu.
Mkuu huyo wa wilaya alitaja miradi mingine itakayopitiwa na kuweka jiwe la msingi kisima cha maji kilichopo Mang'enya Kata ya Genge na kukagua mabweni ya wanafunzi shule ya Livingstone.
Alisema kuwa baada ya Mwenge huo kukagua miradi hiyo utakagua mabanda ya maonyesho katika uwanja wa Jitegemee ambako mwenge huo utakesha mpaka asubuhi.
Kwa upande wake Mratibu wa Mwenge Wilaya ya Muheza, Athumani Komolanya aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea mwenge huo katika barabara ambapo utapokelewa Kijiji cha Mjesani ukitokea wilayani Mkinga na asubuhi yake utakabidhiwa Kijiji cha Masaika ukielekea wilayani Pangani.

No comments:

Post a Comment