WATOTO 5,000 wenye umri wa miaka 10 kushuka chini,
wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), katika
Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.
Mbali ya watoto hao, watu wazima
11,000 nao wameanza kutumia dawa hizo katika kliniki iliyopo hospitalini hapo.
Daktari wa Kitengo cha Kuratibu Wagonjwa wa UKIMWI,
Shani Mwaruka, aliyasema hayo wakati kamati ya kudhibiti ugonjwa huo Manispaa
ya Ilala, ilipofanya ziara katika hospitali hiyo.
Alisema kwa
siku kliniki hiyo uhudumia wagonjwa 250 hadi
300 ambao wanatoka kwenye maeneo
mbalimbali na kudai kuwa, changamoto waliyonayo ni baadhi ya wagonjwa
kutokubaliana na hali waliyonayo pamoja na uchache wa vitendea kazi.
“Watu wengi
hawakubaliani na hali waliyonayo, baba anapokuja kupima afya yake anamficha
mkewe na kuanza kutumia dawa peke yake na wanawake pia hivyo hivyo,” alisema
Dkt. Mwaruka.
Aliongeza kuwa,
kitengo hicho kinafanya jitihada za kuhakikisha wazazi wanawaeleza watoto
wanaotumia dawa hizo wanapokua.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo Bw. Said Kitambuliyo, alisema lengo lao ni kutembelea mitandao yote
na asasi za watu waishio na ugonjwa huo, kusikiliza changamoto walizonazo na
kuangalia kazi wanazofanya.
No comments:
Post a Comment