VIBARUA watatu wa kampuni inayojenga barabara ya China
Communication and Construction Company (CCCC), mkoani Mbeya, wamefariki dunia
kwenye ajali ya gari baada ya lori walilopanda likitoka kuchukua kifusi
kupinduka.
Kamanda wa Polisi mkoani humo,
Diwani Athuman, alisema tukio hilo limetokea jana saa sita mchana katika eneo
la Iganzo, maarufu kama Mwisho wa Lami, barabara ya Mbeya-Chunya.
Alisema gari hilo lenye namba T 405
BWA aina ya
Zhongji mali ya kampuni hiyo, lilikuwa likitoka kuchukua kifusi
katika eneo la Kawetele, ambapo dereva aliyesababisha vifo hivyo jina lake
halikufahamika mara moja baada ya kukimbia.
Aliongeza kuwa, lori hilo
lilipinduka baada ya dereva huyo kushindwa kulimudu kutokana na mwendo kasi
katika eneo lenye kona na mteremko mkali.
Hata hivyo Kamanda Athuman alisema
marehemu wote ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa mkoani
humo, bado hawajatambuliwa.
Alisema katika ajali hiyo kulikuwa
na majeruhi watano kati yao watatu walitibiwa hospitali na kuruhusiwa, wawili
wamelazwa katika hospitali hiyo.
Aliwataja majeruhi wanaoendelea na
matibabu kuwa ni msimamizi wa vibarua hao raia wa China, Don Fung Cheng (38),
aliyejeruhiwa kichwani, pamoja na mtu mwingine ambaye hajafahamika jina
kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Waliotibiwa na kuruhusiwa ni Ayoub
Samson (25), Jelicko Apton(18) na Natifa Ngole (23), wote wakazi wa Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment