31 May 2013

Wanaoita wenzao mafisadi wamkera Pinda

Na Elizabeth Joseph, Dodoma




WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewatahadharisha watu wanaopenda kuwaita wenzao mafisadi pindi wanapowaona wamepata mafanikio kwa kuwa na yeye anatarajia kunufaika na ufugaji wa nyuki.
Alisema hivi karibuni anatarajia kuvuna asali karibu tani moja na mara akianza kuiuza lazima apate faida kutokana na asali hiyo, hivyo Watanzania wenye dhana ya ufisadi kwa wanaopata faida au maendeleo katika shughuli za kujiinua kiuchumi waache tabia hiyo.
Pinda alibainisha hayo juzi mjini hapa wakati akifungua semina ya wakuu wa mikoa na wilaya nchini iliyohusu utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima.
Aliwataka wakuu hao kutafuta njia ya kuwasaidia wafugaji nchini kwa
kuwapa fedha kwakuwa nao ni sehemu ya kilimo pamoja na kuwataka kuwawezesha vijana nchini kwa kuwashauri kuhusu kilimo na ufugaji ili kuwapa ajira na kuwaongezea kipato.
"Lazima tuwatengenezee utaratibu vijana kwa kuwapa ardhi kwa kutenga maeneo maalumu,mbegu na fedha kwa ajili ya kilimo na ufugaji ili vijana waweze kujiajiri na kujipatia kipato," alisema Pinda.
Aliwataka wakuu hao kujiuliza kama kuna mabadiliko ya kipato na kimaendeleo kwa wananchi katika wilaya na mikoa yao tangu walipokabidhiwa kushika madaraka.
"Jiulizeni mmefanya nini katika kuwapandisha kimapato wananchi wenu tangu tumewakabidhi kuwaongoza katika hali moja kwenda hali nyingine na lazima muwe wabunifu katika kuleta mabadiliko na maendeleo kwa wananchi wenu," alisema Pinda.
Hata hivyo aliwataka kuangalia kwa makini suala la mfumo wa malipo ya vocha kwa wasambazaji kwa kuwapatia vocha kwa wakati na kuhakikisha wanasimamia vizuri vocha hizo kwakuwa serikali iliona mfumo huo ndio njia nzuri ya kumwezesha mkulima kupata mbegu bora na kumfikia mkulima bila kuchelewa pamoja na kuhakikisha wanaviingiza vikundi vinavyotambuliwa katika utoaji ruzuku ili kuondoa udanganyifu katika malipo hayo.

No comments:

Post a Comment