16 May 2013

Walimu wauponda mfumo wa elimu nchini

Na Yusuph Mussa, Lushoto


 BAADHI ya walimu wilayani Lushoto wameifananisha elimu ya Tanzania kama maghorofa mabovu yanayojengwa jijini Dar es Salaam, kwani inazidi kushuka kutokana na mfumo mbovu wa mitaala na uingizaji holela wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia shuleni.
Wakizungumza juzi kwenye mkutano wa wakuu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Bumbuli, ulioandaliwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba waliitaka Serikali ishirikishe wadau kwenye
mitaala.
"Kama mchakato wa Katiba Mpya unavyoshirikisha wadau, vivyo hivyo utungaji ama uanzishwaji wa mitaala mipya iwashirikishe wadau ili kupata mitaala itakayokubalika au sivyo elimu yetu itaendelea kuwa kama maghorofa ya Dar es Salaam.
"Itazidi kuporomoka kwa vile haina misingi mizuri. Hivi inakuwaje mtoto wa darasa la kwanza anakwenda shuleni na madaftari tisa, turudishe utaratibu wa K tatu yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu" alisema Mratibu wa Elimu Kata ya Soni, Luth Msagati.
Mratibu wa Elimu Kata ya Milingano alisema mitaala iliyopo kwa sasa hata walimu hawaijui, hivyo ni vigumu mwalimu kumfundisha mwanafunzi akaelewa, huku akisema changamoto nyingine ni kuwaingiza sekondari wanafunzi waliopata alama 70.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwamongo, Anthony Kihiyo alisema kwa Serikali kuruhusu wanafunzi wa shule za kata na zile za Mtakatifu kufanya mtihani mmoja ni sawa na kumpambanisha Francis Cheka na mgonjwa aliyelazwa Hospitali ya Muhimbili.
"Wanafunzi wa shule za kata kufanya mtihani mmoja na wale wa shule binafsi ni kuwaonea. Hata mabondia uzito wao unapimwa na unatakiwa ulingane ndipo wapigane," alisema Kihiyo.
Makamba alisema pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza kisa cha matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana, bado walengwa ambao ni walimu hawajapewa nafasi ya kutoa maoni yao juu ya suala hilo.
"Sauti ya mwalimu haijasikika zaidi ya wanasiasa na makundi mengine, lakini walimu hasa ndiyo wanajua kitu gani kimefanya wanafunzi wamefanya vibaya, sababu ndiyo wanakaa na wanafunzi hawa kati ya saa nane hadi tisa," alisema Makamba.
Makamba aliungana na walimu kwa kusema mitaala isitegemee mapenzi ya waziri aliyepo madarakani ama Serikali inayoongoza dola, bali iwe ni suala la kitaifa ambapo kila Serikali ama waziri atakaekuja atafuata mitaala hiyo.

No comments:

Post a Comment