UMEME kupita
juu ya Kijiji cha Wanga kilichopo Kata ya Mgwashi wilayani Lushoto na wao
kushindwa kuwekewa trasfoma ili wapate huduma hiyo kumekigharimu Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa wananchi kuamua kumchagua Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji
hicho kupitia CHADEMA.
Wakizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara
ulioandaliwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa
Bumbuli, January Makamba wananchi walisema kupitisha nyaya za
umeme juu na
kuwapelekea wanakijiji wenzao wa Mgwashi ni kuonesha Serikali ya CCM haiwajali.
"Umeme kupita juu kwa juu kwenda Kijiji cha
Mgwashi na kutuacha sisi, tumeona Serikali haitujali. Lakini pia tunachangishwa
michango mara mbili mbili, kwani tulikamilisha boma (darasa) la Shule ya
Sekondari Handeni.
"Awali tulijenga likakamilika kwa kutoa
kila mtu sh. 5,000, lakini kwa vile lilijengwa chini ya kiwango ikabidi
tuchangishwe tena sh. 3,000. Wananchi wananyanyaswa kwa kuambulwa (kushikwa
faini) kuku ili kujenga tena boma hilo," alisema Athuman Amir.
Makamba aliwataka wananchi wawe na subira kwani
ipo mikakati ya kufikisha umeme kwenye kata kadhaa kwenye Halmashauri ya
Bumbuli ikiwemo eneo hilo.
Pia alisema
kwa kupata halmashauri wataweza kuipandisha barabara ya Mbelei- Mgwashi-
Milingano- Mashewa kuwa chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS).
No comments:
Post a Comment