Na Suleiman Abeid,
Kahama
KATIKA
hali isiyo ya kawaida, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyasubi, iliyopo Wilaya
ya Kahama, mkoani Shinyanga, wamepiga kura za siri ili kuwafichua walimu wenye
tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi wao shuleni hapo.
Uamuzi wa kupigwa kura hizo ulifikiwa
hivi karibuni kwenye Kikao cha Baraza la Shule la Watoto ambacho kiliitishwa
kwa lengo la kujadili vurugu zilizokuwa zikijitokeza shuleni hapo na
kusababisha baadhi ya walimu kupigwa.
Kikao hicho kiliitishwa na Mratibu wa
Mradi wa Haki Yangu Sauti Yangu, mkoani humo, Bw. Gerald Ng’ong’a na kubaini
kuwa, sababu moja wapo iliyochangia vurugu hizo ni baadhi ya walimu kufanya
mapenzi na wanafunzi wao.
Inadaiwa hali hiyo pia imechangia
wanafunzi wengi waliomaliza kidato cha
nne shuleni hapo kupata matokeo mabaya,
kuporomoka kwa kiwango cha elimu kutokana na walimu kutotimiza wajibu wao
kikamilifu.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza
katika kikao hicho, walisema chanzo cha vurugu ni wanafunzi wa kiume kuwa na
uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wa kike hivyo wanachukizwa na kitendo cha
baadhi ya walimu kutembea na wapenzi wao.
Walisema kutokana na hali hiyo,
wanafunzi wa kiume waendapo mitaani hujiunga na vikundi vya wahuni ambao
huchukua hatua za kuwateka na kuwapiga walimu wao ili kulipa visasi.
Hata hivyo, wanafunzi hao walipotakiwa
kuwataja walimu wenye tabia hiyo waliomba ufanyike mchakato wa upigaji kura za
siri ambapo kazi hiyo ilisimamiwa na walimu pamoja na wazazi walezi ambao
walishiriki kikao hicho.
Kura hizo ziliwataja majina ya baadhi
ya walimu wenye tabia hiyo na majina ya wanafunzi wanaoshiriki kufanya nao
mapenzi lakini hazikutangazwa kwa kuwa ni siri na zitawasilishwa kwa uongozi wa
shule ili wahusika waitwe na kuonywa.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanafunzi
shuleni hapo walilalamikia kitendo cha walimu wao kuwapa adhabu kubwa
zisizolingana na makosa wanayoyafanya wakitolea mfano wa adhabu ya kugaragazwa
chini kwa kosa la kutokutoa ada ambalo walisema si kosa lao bali ni la wazazi.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Ng’ong’a,
aliwashauri wazazi, walezi kuhakikisha wanafanya vikao vya mara kwa mara ili
waweze kurejesha hali ya amani na utulivu shuleni hapo.
"Nimesikitishwa kusikia miaka
minne hamjaitisha kikao chochote cha Bodi ya Shule wala cha wazazi, hali hii
inachangia mambo mengi kutopatiwa ufumbuzi wa haraka pale yanapojitokeza.
"Ni muhimu kuwa na vikao vya mara kwa mara pamoja na Baraza
la Shule la Watoto ili kutoa fursa ya kusikiliza kero mbalimbali
walizonazo," alisema Bw. Ng’ong’a.
No comments:
Post a Comment