KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya
Bunda, mkoani Mara Jonas Sariro, ametoa onyo kwa viongozi wa Chama cha Walimu
nchini (CWT), wilayani humo na kudai kuwa, CCM ina jukumu la kuwasimamia
watumishi wa Serikali ili waweze kutekeleza sera na ilani ya chama.
Sariro ametoa
onyo hilo kutokana na madai ya CWT wilayani humo kuilalamikia CCM wakidai
viongozi wake wanafanya kazi za Serikali kwa kukagua utendaji wa walimu
shuleni, kuwafokea na kutishia kuwafukuza kazi au kuwahamisha.
CWT walidai
kuwa, hoja ya viongozi wa CCM ni juu ya chama ambacho ndicho kinachoongoza dola
kuwajibika kuwalipa mishshara walimu.
Alisema CCM ipo
tayari kuwachukulia hatua walimu wote ambao
watashindwa kuwajibika na kuwataka
viongozi wa CWT waache kuwapotosha wanachama wao (walimu).
Akizungumza na
waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Sariro alisema madai ya CWT hayana maana
kwani Mwenyekiti wa CCM wilayani humu, Bw. Chacha Gimanu, yuko katika ziara ya
kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
Aliongeza kuwa,
ziara hiyo inafanyika katika kata zote wilayani hamo ili kutoa mapendekezo
mbalimbali katika maeneo ambayo yatabainika kuwa na kasoro za kiutendaji si
kutoa vitisho.
“Katika ziara
hizi, Ofisa Mtendaji wa kata ambaye ndiye Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya
kata, husoma taarifa ya utekelezaji wa ilani akisaidiana na wakuu wa idara
mbalimbali katika kata ikiwemo idara ya elimu.“Sisi hatuwahoji walimu kama
inavyodaiwa, CWT inataka kuacha malengo yake na kugeuka kuwa chama cha siasa.
Naomba chama
hiki kisimamie wanachama wake ili wawajibike ndipo wadai masilahi yao,”
alisema.
Hivi karibuni,
Mwenyekiti wa CWT wilayani humo, Bw. Francis Ruhumbika, aliituhumu CCM kuwa Mei
22 mwaka huu, Mwenyekiti wake wa Wilaya, Bw. Gimanu alifika katika Shule ya
Msingi Nyamuswa ‘A’, kuwaita walimu, kuwahoji na kuwatishia kuwa atawahamisha
vituo vya kazi.
“Sisi viongozi wa CWT wilaya ya Bunda tunasema kuwa,
Mwenyekiti wa CCM wilayani hapa si mamlaka ya nidhamu ya walimu...viongozi wa
kisiasa wafanye mambo ya siasa,wasigeuke kuwa mamlaka ya kuwajibisha walimu,”
alisema.
No comments:
Post a Comment