MGOGORO
wa wakulima wa chai, Chama cha Wakulima wa Chai Usambar a (UTEGA) na mwekezajiShadadMullah
umeingia sura mpya baada ya wakulima hao kuamua kung’oa zao la chai na kupanda
mahindi. Wakulima hao wanadai kilimo cha chai kimekuwa ni sawa na biashara
haramu kwao. Hayo waliyabainisha kwa nyakati tofauti juzi nje ya uzio wa
Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto
wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi. Walisema, wao kulima chai na
kuiuza kwenye kiwanda bila kulipwa vizuri wakati ni wabia ni sawa na kero.
“Mwandishi angalia upande ule tumeamua kung’oa chai na kupanda mahindi, tumeona
kwetu hii ni biashara haramu, kwani hatufaidiki nayo pamoja na kwamba sisi ni
wabia kupitia Chama wa
Wakulima cha UTEGA,” alisema Juma Sheshe. Naye mkulima
Mustafa Soa alisema, wamenyanyasika kwa miaka 13 tangu UTEGA waingie ubia na
mwekezaji huyo huku wakiwa hawajui mapato na matumizi wala hisa zao kwenye
kiwanda hicho ni kiasi gani. Aidha, Sauli Makasi alisema wameanza kuzalisha kwa
faida kwenye kiwanda hicho miaka nane iliyopita lakini hakuna chochote
wanachopata huku wakijiuliza wao wapo ubia kati ya wakulima na mwekezaji,
lakini mbona kuna mashirika yanaundwa katikati yake. “Sisi tumeingia ubia na
mwekezaji, lakini kuna mashirika yameundwa katikati yetu kutunyonya, mfano kuna
Lushoto Tea Estate na pia kuna Mponde Tea Estate haya yanafanya kazi gani,”
alisema Makasi. Hata hivyo wakulima hao walikanusha kufanya fujo kwenye kiwanda
hicho kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kupitia Jeshi la
Polisi. Walidai sababu za kutokufanya fujo katika kiwanda hicho wana hisa
kwenye zao na wameamua kukilinda usiku na mchana kusitokee kitu ama kuingia
kiwandani hapo. “Tunalinda mali zetu na ndiyo maana tupo hapa. Angalia kiwanda
kipo salama na hakuna kitu kilichoharibiwa ndani ya kiwanda hiki,” alisema
Almas Shemshami. Mmoja wa mgambo wanaolinda kiwanda hicho, Festo Ngoda alikiri
kutoharibiwa mali yoyote kiwandani humo ila yeye alipigwa na ubapa wa panga
baada ya kuonekana yupo nyuma ya kiwanda hicho akihisiwa kama anataka kutoroka.
Akizungumza na waandishi wa habari mwekezaji Mullah alisema, ndani ya mgogoro
huo kuna mambo ya kisiasa huku akitupa lawama kwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli,
January Makamba kuwa hajawaonesha ushirikiano katika kumaliza kero na
changamoto za wakulima wa chai. “Tangu mwaka 2008 tumekuwa na matatizo ya
kukiendesha kiwanda, baada ya msitu wetu wa miti wa Sakare wilayani Korogwe kwa
ajili ya kuni za kukausha chai kuzuiwa tusivune na sasa wakulima wanadai
hawataleta chai. “Suala hili limechangiwa na Mbunge January kushindwa kutoa
ushirikiano kwetu, lakini tunaamini angekuwa karibu yetu isingefikia hapa,
lakini sisi tunasema tupo pale kama wabia. Ni baada ya Serikali kubinafsisha
kiwanda mwaka 1998 na sisi kuingia ubia na wakulima,” alisema Mullah.
Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi akiwa Dodoma, Makamba alisema
sio kweli kuwa ameshindwa kutoa ushirikiano bali amekwishafanya vikao na
mwekezaji huyo kupitia familia yake ikiwemo kuwaita ofisini kwake Dar es Salaam
ili kujua mustakabali wa chai na wakulima wao. “Nimekaa na baba yake mzee
Mullah na kaka yake Yusuph zaidi ya mara tatu. Tumefanya makubaliano kadhaa
kuhusu namna ya kutatua tatizo, lakini hawakutekeleza. Pia tulikaa ofisini
kwangu na mzee Mullah, Yusuph na Mkurugenzi wa Bodi ya Chai nchini (Assenga)
hakuna ufumbuzi uliopatikana. “Kuna kikundi kinaitwa Ushirika walikuwa
hawapeleki majani pale na kiwanda kikawa hakipati majani, Yusuph akaniambia
nikawashawishi Ushirika wapeleke majani, wakaanza kupeleka hadi leo. Anataka
ushirikiano gani,” alihoji Makamba. Hata hivyo kiwanda hicho kimeingia kwenye
mgogoro baada ya mkutano uliofanyika Mei 26, mwaka huu kati ya wakulima na
Makamba ambapo wakulima walitoa azimio la kutokiuzia malighafi kiwanda hicho
baaada ya kuona hawapati faida.
No comments:
Post a Comment