USHIRIKIANO na mwamko wa wakulima walioungana katika
vikundi kutekeleza mradi wa Mpango wa Maendeleo vijijini; katika mwambao wa
Pwani ya Tanzania (CRSPT); unaotekelezwa na Aga Khan Foundation, katika Wilaya
ya Newala, umewafurahisha, viongozi katika kata ya Mcholi ya kwanza,
walioshiriki siku ya wakulima kijijini, Chiunjila, anaripoti Godwin
Msalichuma, Newala.
Hayo yalijitokeza kijijini hapo hivi
karibuni, ambapo diwani Selemani Kaisi, alipopewa fursa ya kuzungumza na
vikundi vya wakulima takribani 87, wanaume 61 na wanawake 26, walikusanyika
katika siku yao, ili kujifunza pamoja mambo muhimu na changamoto zinazowakumba
katika mradi huo wa kilimo cha mpunga na ufuta.
“Nimeridhishwa sana na utekelezaji wenu
wa mradi huu kwa ushirikiano na kwa kweli unanitia moyo kuona haya yakifanyika
kwa umoja na nguvu ya pamoja, niseme kuwa mmeshakuwa wataalamu sasa, ninaimani
mnaweza kuendelea hata bila ya wafadhili kuwepo” alisema Kaisi na
kuongeza kwa
kuwaasa:
Waendelee na utaalamu huo walioupata
kuboresha kilimo cha mpunga na ufuta na pia kuhifadhi elimu hiyo kwa faida ya
vizazi vyao vijavyo.
Alisema, amefurahishwa na kusikia
kuwa awali kabla ya mradi wakulima walikuwa wanavuna mpunga katika hekta moja
magunia manne mpaka matano, lakini sasa wanafikisha magunia 25 mpaka 40.
Aidha, aliwaomba kuwa macho na
walanguzi wa mazao wakati wa mavuno; kwani mbinu wanazopewa na asasi hiyo ya
kimataifa, ni nzuri ya kukusanya na kuhifadhi pamoja, wakisubiri bei nzuri
itakapofika katika zao hilo la mpunga.
“Nawaomba muwe macho na walanguzi wa
mazao yenu, wasije wakawarubuni wakati wa mavuno tukauza mpaka mbegu; nawasihi
mtumie hivyo vikundi vya kuweka na kukopa (Vicoba), yaani ‘wekeza boresha
maisha’ hapo tukiweka akiba nadhani kilimo kitakuwa na manufaa zaidi,” alisema
diwani huyo.
Naye, Ofisa Kilimo na Maendeleo ya
Mifugo katika Wilaya ya Newala (DALDO), Alford Mpanda, alisema, baada ya kuona
maendeleo mazuri ya kilimo cha mpunga kijijini Chiunjila, alidai amegundua kuwa
kumbe kuna mazao ambayo wakulima, wanaweza kuzalisha bila mikikimikiki kama
ilivyo kwa zao la korosho, ambapo lina gharama kubwa katika kuandaa shamba na
kupata mapato yake.
“Inanipa moyo sana na nguvu kuona
kuwa kumbe kuna mazao kama mpunga na ufuta yanachukua muda mfupi na gharama
ndogo k u y a z a l i s h a , h a t a h a k u n a mikikimikiki ukilinganisha na
zao la korosho,” alisema Mpanda.
Hata
hivyo alifurahishwa na kuridhishwa kuona kuwa hata mapato kwa wakulima
yameongezeka kutoka magunia matano kwa hekta mpaka magunia 40, ambapo
aliwashauri kuongeza bidii katika uzalishaji, kwani pia uzalishaji wao
unaongeza pato la halmashauri na Taifa kwa ujumla wake.
No comments:
Post a Comment