31 May 2013

Mtatiro kuzindua kampeni udiwani Muheza

Na Mwandishi Wetu, Muheza


 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),Julius Mtatiro anatarajiwa kuzindua kampeni za udiwani katika Kata za Genge na Tingeni zilizoko wilayani Muheza Mkoa wa Tanga.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa, Nuru Awadh Bafadhili alisema jana kuwa uzinduzi huo utafanyika siku mbili ambapo katika Kata ya Genge utafanyika kesho na Kata ya Tingeni itakuwa Juni 2.
Alisema mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu huyo yatafanyika katika Kijiji cha Kerenge Kata ya Tingeni na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo.
Wakati huo huo,Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Muheza mkoani
Tanga kimepata pigo baada ya wanachama wake 72 wa Kata ya Pande Darajani kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).
Wanachama hao walikabidhiwa kadi hizo juzi na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake CUF Taifa, Nuru Awadh Bafadhili katika mkutano wa kuhamasisha uhai wa chama hicho uliofanyika katika kata hiyo.
Akikabidhi kadi kwa wanachama hao wapya aliwataka wasiogope vitisho kwani vitakuwa vingi hasa nyakati hizi za chaguzi ndogo, lakini aliwataka waendelee na kuunga mkono CUF yenye ‘Dira ya mabadiliko’na kusisitiza kuwa hataweza malaika kuwaambia kuwa CCM imeshindwa kuwaletea Watanzania maisha bora.
Alisema katika kipindi cha miaka 52 ya uhuru bado Watanzania hawana uhakika wa maisha yao ya kila siku na kuwataka kuunga mkono hicho ili kilete mageuzi ya kweli ndani ya taifa.
Bafadhili aliwataka wanachama hao kuendelea kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kushinda katika chaguzi ndogo za udiwani na uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Katibu wa CUF Wilaya ya Muheza, Juma Nindi na Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya, Omari Sesunga waliwataka wanachama hao kuendeleza mshikamano kwani dhamira ya chama hicho ni kushika dola mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment