30 May 2013

VICOBA yakabidhi simu bure kwa wanachama

Na Heri Shaaban


 WANACHAMA w a Vikundi vya Kuweka na Kukopa (VICOBA) wamekabidhiwa simu za mkononi bure,ili waweze kuweka fedha zao kwa njia ya kisasa na kuachana na mtindo wa utunzaji fedha kwa njia ya masanduku.
Hatua hiyo ya kuwakabidhi simu hizo ilizinduliwa Dar es Salaam jana na Makamu wa kwanza wa Rais wa Vicoba Taifa Scholastica Kevela.
Akizindua kampeni hiyo kwa wana Vicoba, Bi. Kevela alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza taarifa za upotevu wa fedha na kuwarahisishia uwekaji wa fedha katika mazingira mazuri.
“Hata kama simu ya mkononi itaibiwa lakini fedha zilizokuwepo hazitaweza kuchukuliwa labda muhusika awe anafahamu namba ya siri na hivyo leo nitakabidhi kwa vikundi vya
Midizini A, Midizini B na Minazi Mirefu na juhudi hizi zitaendelea,” alisema.
Alisema vikundi vingi bado vinaendelea kuweka fedha kwenye vibubu na kwamba hali hiyo ni hatari kwani inatoa mwanya kwa vibaka na vishawishi kwa wale wanaotunza vibubu hivyo.
“Sasa hivi tunahamasisha electronic vicoba (utunzaji fedha kwa njia ya mtandao) mnaweka fedha zenu kwa njia ya M-Pesa, kwa sababu wanachama wengi wamekuwa wakilalamika kila siku kuibiwa fedha kutokana na utunzaji wa kwenye vibubu," alisema Kevela.
Makamu huyo wa Rais wa Vicoba, alisema pia baadhi ya watu wamekuwa matapeli kwa kuchangisha fedha watu na kutokomea nazo hivyo akawataka wanachama wa vicobakutunza fedha zao wenyewe.
Pia aliwataka wanachama wa vikundi hivyo kuacha majungu na kufanya kazi kwa bidii ili kujikomboa kiuchumi.
Naye Mratibu wa Ujasiriamali VicobaTaifa, Flora Masalu, alitoa wito kwa wanachama wa vikundi hivyo kutokurupuka kwenda kuchukua mikopo bila kuwa na biashara ya kufanya.

No comments:

Post a Comment