30 May 2013

Musai chafaidika na mradi wa samaki

Na Mercy James, Mbarali


 KIKUNDI cha Muungano wa Ufugaji Samaki Igomelo (MUSAI) kilichopo kijiji cha Igawa wilayani Mbarali mkoani wa Mbeya, kimeanza kunufaika na mradi wa ufugaji samaki katika mabwawa yaliyopo katika eneo la umwagiliaji la Igomelo na kujipatia zaidi ya sh. milioni 2.3.
Kikundi hicho ambacho kilianza mwaka 2009 kikiwa na wanachama 30 na sasa wamebaki 19, kimetumia nguvu zao kwa asilimia 20 na serikali kupitia mfuko wa DADPS kuchangia asilimia 80 ya mradi huo, ambapo wafugaji hao wamevuna jumla ya kg 170, katika awamu ya kwanza na awamu ya pili wamevuna kg 200 na kupata jumla ya kg 370.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Musai, Abdallah Jumma alisema licha ya
kuvuna samaki hao wanategemea kupandikiza vifaranga 9,600 katika mawawa hayo na ameeleza baadhi ya changamoto zinazowakabiri na mtazamo wao wa baadaye kuwa ni kuzalisha samaki kwa wingi ili kukuza kipato katika kaya za wanakikundi.
Kaimu Ofisa Idara ya Uvuvi wilaya alisema, pamoja na kutoa elimu ya ufugaji pia idara hiyo inasimamia upandikizaji, utunzaji hadi kufikia wakati wa kuvuna na mipango ambayo wameiweka katika kuhakikisha mabwawa 300 yaliyopo wilayani humo yanakuwa na mazao ya samaki ili kukuza uchumi wa kaya za wanavikundi waliopata mafunzo.
Augustine Lawi, Mkuu wa Idara ya Uvuvi na Mifugo amesema, awali mafunzo hayo yalitolewa na wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ambapo wananchi walielimishwa kuhusu ufugaji na utunzaji wa samaki bwawani katika kuongeza uzalishaji wa vifaranga.

No comments:

Post a Comment