17 May 2013

Tatizo la ajira kwa vijana, Lowassa ataka mjadala

Na Mwandishi Wetu


 WAZIRI Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, ametoa wito wa kuwepo mjadala mpana ambao utazungumzia tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Bw. Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa kitabu ambacho kinazungumzia na kutathmini mzozo wa kiuchumi duniani kwa kuiangazia Tanzania.
Alisema ni muhimu wadau wote wakiwepo wasomi, wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi wasio na ajira hususan vijana, kushiriki mjadala huo na kutoa mapendekezo ili tatizo hilo lipatiwe ufumbuzi.
"Nafurahishwa kuona mmoja wa wana zuoni mashuhuri wa masuala ya
uchumi nchini, Dkt. Honest Ngowi, ametumia rasilimali zake na muda wake kufanya utafiti.
“Ameandika kwa kina mdororo wa uchumi wa mwaka 2008 kwa mtizamo wa Tanzania,” alisema Bw. Lowassa na kumpongeza msomi huyo kwa kazi aliyoifanya.
Bw. Lowassa ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipigia kelele tatizo la ajira kwa vijana, alisema kutokana na mdororo wa uchumi duniani mwaka 2008 na ule uliozikumba mataifa yanayotumia sarafu ya euro mwaka 2010, tatizo la uhaba wa ajira linaweza kutatuliwa kwa kuimarisha soko la ndani.
“Mdororo wa mwaka 2008 na 2010, ulisababisha ongezeko la tatizo la ajira hapa kwetu...bidhaa zetu kama vile mazao na madini, zinategemea sana soko la nje,”' alisema na kuongeza mdodoro huo kwa mujibu wa takwimu, ulisababisha watu 48,000 kukosa ajira.
Alisema tatizo la ajira Tanzania ni kubwa kwa uchumi wa kijamii hivyo ni bomu linalosubiri kulipuka na madhara yake ni mabaya kwani vijana wanaweza kutumika kwa namna mbaya kwa sababu hawana cha kupoteza.
“Tukumbuke msemo unaosema kichwa kisichokuwa na fikra yoyote basi ni karakana ya shetani," alisisitiza.
Aliwaomba wanazuoni kuongeza jitihada zao katika kuzalisha ufahamu kutokana na tafiti zao na kwenda mbele zaidi kwa kutoa machapisho ya tafiti zao na kuyasambaza.
Bw. Lowassa alisema sambamba na juhudi hizo, upo umuhimu wa Serikali kuongeza ufadhili katika sekta ya utafiti, uchapishaji na usambazaji wa ufahamu unaotokana na tafiti mbalimbali.
“Naiomba Serikali iboreshe mazingira ya uwekezaji kwa wachapishaji na wazalishaji majarida na vitabu ili kuwa na kazi za kiwango cha juu kutoka nchini,” alisema Bw. Lowassa na kuongeza kuwa, sekta hiyo ni moja wapo ya mikakati mizuri ya kutoa ajira.

No comments:

Post a Comment