Goodluck Hongo na Mariam
Mziwanda
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeunga mkono uamuzi wa
Jukwaa la Katiba nchini kutaka kuifikisha mahakamani Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Mwenyekiti wa
chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema chama
hicho kinasubiri rasimu ya Katiba ili waweze kutoa msimamo wao juu ya mchakato
huo.
Aliongeza kuwa,
Jukwaa la Katiba lipo huru kuifikisha tume hiyo
mahakamani kutokana na sababu
zao lakini CUF inasubiri rasimu hiyo, kuipitia na kutoa msimamo wao.
Aliongeza kuwa,
chama hicho kinaungana na Watanzania wengi wanaoonesha shaka juu ya mchakato
huo kwani katiba ambayo haitakuwa na misingi imara ya kidemokrasia na
isiyotokana na maoni ya Watanzania, lazima ikataliwe.
“Kama itatokea
hivyo, CUF tutawahamasisha Watanzania nchi nzima kuikataa katiba isiyotokana na
maoni yao, hata sisi tulichakachuliwa wakati mgombea wetu akiwa ameongoza
wagombea wengine saba,” alisema.
Alisema Baraza
Kuu la CUF linaitaka tume hiyo kuweka utaratibu wa kuyafikia makundi yote yenye
mahitaji maalumu wakiwemo walemavu na wanawake.
Akizungumzia
maazimio ya baraza hilo ambalo lilikutana kwa siku mbili, alisema lilijadili
mambo mbalimbali ukiwemo uchaguzi mdogo Jimbo la Chambani- Pemba.
“Baraza
limekubaliana kwa kauli moja kumteua Bw. Yusuf Salum Hussein kuwa mgombea wetu
katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Juni 16, mwaka huu, awali walijitokeza
watu 12 kuwania nafasi hii ili wateuliwe na baraza kugombea,” alisema.
Wakati
huo huo, Kamati Maalumu ya Katiba Mpya ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu,
imeitakaSerikali kuwa sikivu na kufanyia marekebisho kasoro zilizopo katika
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge la Katiba.
Kufanyika kwa
marekebisho hayo, kutaiwezesha nchi kupata Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa
ya Watanzania.
Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Dkt. Khoti Kamanga, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, kama kasoro hizo
zitarekebishwa, Katiba Mpya yenye masilahi ya wananchi itapatikana.
Alisema kamati
hiyo imebaini uundwaji wa Bunge la Katiba lenye wajumbe 166 sawa na theluthi
moja ambalo halizingatii masilahi ya nchi na watu wake kwa kuwa na Bunge la
asilimia 72 ya wabunge kutoka Bara na Zanzibar.
Aliongeza kuwa,
kutokana na hali hiyo mfumo uliopo unaondoa dhamira ya kupata katiba bora
ambapo mfumo uliopo wa uundwaji Bunge hilo unawaondolea haki ya kushiriki walio
nje ya mfumo wa vyama vya siasa na ambao si wabunge.
“Kama
marekebisho yatafanyika, tutapata Katiba Mpya waitakayo wananchi ambao watakuwa
walinzi ambapo watawala au viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa
katiba, watakuwa wanyenyekevu wa kutosha kwa wananchi.
Dkt. Kamanga
alisema, uundaji wa Bunge hilo unaweza kufanyika kwa kufanya uchaguzi wa
kidemokrasia na kupata wajumbe ambao watachujwa na vyombo vingine au kutumia
makundi ya kijamii yanayowakilisha masilahi ya aina zote ili kupata mwafaka wa
kitaifa.
Kamati hiyo
imeshauri Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi kutoa wajumbe wasiozidi
theluthi moja na theluthi mbili zilizobaki kuwaachia wananchi walio nje ya
mfumo wa vyama vya siasa kwa utaratibu utakaoruhusu uchaguzi miongoni mwa
makundi ya kiraia.
Aliwaomba
wananchi kuunga mkono mapendekezo hayo ili kutoa kipaumbele kwa Serikali
kuwapatia raia wake haki ya kuandaa katiba waitakayo.
No comments:
Post a Comment