30 May 2013

PPF yatumia mil. 680/- kusomesha wanafunzi

Na Mashaka Mhando, Tanga


 MFUKO wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) unaoshiriki kwa mara ya kwanza Maonesho ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika Jijini Tanga, hadi kufikia Desemba mwaka jana, umetumia kiasi cha shilingi milioni 682.9 kusomesha wanafunzi wapatao 1,333 nchini.
Akizungumza na gazeti hili, katika mahojiano maalumu Ofisa Uhusiano wa mfuko huo, Janet Ezekiel, alisema kuwa fedha hizo wamezitumia kusomesha wanafunzi hao kupitia fao la elimu ambalo wanasaidia kuboresha na kusaidia suala la elimu kwa wanachama wake.
Ofisa Uhusiano huyo, alisema mbali ya fao hilo la elimu pia mfuko huo hadi kufikia Machi 31 mwaka huu tayari walikuwa na jumla ya wanachama wapatao 219,000 uliosababisha mfuko huo
kufikia thamani ya shilingi trilioni 1,168.
“Tupo hapa katika maonesho haya ya biashara ya kimataifa mjini Tanga ambako pamoja na mambo mengine, tunawapa taarifa mbalimbali wanachama wetu ili waweze kujua namna bora ya mfuko wao unavyoendeshwa baada ya kuingia katika teknolojia za mitandao na simu za mikononi ikiwa ni kuwapa taarifa wanachama,” alisema.
Akizungumzia suala la uwekezaji Ofisa huyo, alisema kuwa mfuko huo umejikita katika kujenga vitenga uchumi ambapo hadi sasa miji ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wameweza kujenga nyumba kwa ajili ya ofisi, mahoteli na nyumba za kulala wageni.
Alisema mpango uliopo sasa ni kusambaza huduma hiyo katika miji mingine hapa nchini ambayo tayari wamefanya utafiti utakaowezesha kuwa na vitega uchumi na kwamba hivi karibuni wataanza kujenga mradi wa nyumba mkoa wa Mtwara.
Kuhusu kutoa mikopo, ofisa uhusiano huyo alisema kuwa mfuko huo hadi kufikia Mei, mwaka huu tayari wameweza kukopesha vyama vya kuweka na kukopa (Sacco’s) zipatazo 41 hapa nchini kiasi cha shilingi bilioni 55 ambazo zitasaidia wanachama wake.
Mfuko ulianza mpango wa kukopesha saccos za wanachama wake katika maeneo ya kazi mwaka 2004, mpango huu umeleta tija kubwa...maendeleo haya yamechangiwa kwa urahisi na masharti ya kupata mkopo na riba nafuu inayotozwa kwenye mkopo pamoja na muda wa kutosha uliotolewa kurejesha mkopo,” alisema Jannet.

No comments:

Post a Comment