Na Patrick Mabula, Shinyanga
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, linamshikilia askari polisi mstaafu Bw. Samson Bwire (55), mkazi wa Nyasubi, mjini Kahama, kwa kosa la kufanya mauaji ya kinyama.
Bw. Bwire amefanya mauaji hayo kwa mtoto Devota Gerad (4), ambaye alifia Hospitali ya Wilaya hiyo wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake kwa kumpa matibabu.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Evarsti Mangalla, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 10 jioni nyumbani kwa mtuhumiwa, eneo la Nyasubi.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kati ya mtuhumiwa na mama wa mtoto huyo Bi. Hapness Elias (27).
“Mama wa marehemu ni shemeji wa mtuhumiwa...alikuwa mke wa mdogo wake ambaye
amefariki dunia, alikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa akiwa na marehemu ili kusalimia.
“Akiwa hapo, mtuhumiwa alikuwa akimlazimisha Bi. Elias ili amrithi kimapenzi...huyu mama alikuwa akimkatalia siku nyingi ndipo mtuhumiwa alianza kumtukana hivyo kutokea ugomvi uliosababisha akimbie na kumuacha mtoto wake akiwa amelala kitandani,” alisema Kamanda Mangalla.
Aliongeza kuwa, kutokana na hasira mtuhumiwa alichukua panga na kuanza kumshambulia marehemu katika sehemu mbalimbali za mwili wake ambazo ni kichwani, mkononi, usoni na miguuni akiwa amefunga mlango chumbani.
Kutokana na kelele za mtoto huyo, majirani walifika eneo la tukio lakini walishindwa kumuokoa marehemu hivyo waliamua kwenda kutoa taarifa polisi ambao walifika na kuvunja mlango.
Polisi walimchukua mtoto huyo na kumkimbiza hospitali akiwa na majeraha makubwa ambapo wananchi walionesha hasira zao kwa kumshambulia mtuhumiwa ambaye aliokolewa na polisi.
“Wakiwa njiani kwenda kituo cha polisi tena kwa mwendo kasi, mtuhumiwa aliruka, kudondoka kwenye lami na kuumia vibaya ambapo hivi sasa amelazwa hospitalini hapo chini ya ulinzi,” alisema Kamanda Mangalla.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Joseph Fwoma, alisema madaktari na wauguzi walifanya jitihada kubwa za kuokoa maisha ya marehemu lakini alifariki saa tatu usiku.
No comments:
Post a Comment