Cornel Antony, Mtwara
WAFANYABIASHARA wengi mkoani Mtwara, jana walifunga biashara zao wakidai kupewa taarifa zilizowataka wakae katika televisheni zao ili kuangalia Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/14, kama itafafanua jinsi watakavyonufaika na gesi asilia.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini maduka ya dawa muhimu yaliyopo Mtwara Mikindani na Soko Kuu la Mkoa yalikuwa yamefungwa ambapo Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika maeneo mengi.
Kutokana na hali hiyo, mabasi mengi kutoka mikoani ambayo yalikuwa yakiingia saa
saba mchana, yalibadilisha ratiba na kuingia jioni wakihofia vurugu zinazoweza kutokea.
Juzi jeshi hilo liliwataka wakazi wa Mkoa huo kuendelea na shughuli zao kutokana na teteza za kutokea vurugu za kudai haki ya kunufaika na gesi asilia.
Mkazi wa Mtaa wa Chikongola, katika Manispaa hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema wao hawapingi gesi hiyo kusafirishwa nje ya Mkoa huo bali wanachohitaji ni kujua hatma yao jinsi wanavyoweza kunufaika nayo.
Wachungaji
Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa, Serikali imeshauriwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuwakamata mara moja baadhi ya wanasiasa ambao huchochea vurugu na kuharibu amani mkoani Mtwara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuhimiza Amani, Maadili na Haki za Binadamu kwa Jamii kutoka madhehebu mbalimbali ya dini nchini, Mchungaji William Mwamalanga, aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi katika vijiji vya Wilaya ya Tandahimba na Newala, mkoani humo.
Alisema lengo la wachochezi hao ni kuhujumu maendeleo ya wana Mtwara, Taifa na kuonya kuwa ni jambo la hatari wanasiasa kupanda chuki kwa wananchi wakitumia kigezo cha kuzuia gesi isisafirishwe kwenda jijini Dar es Salaam.
Aliufananisha uchochezi huo na unafiki wa kishetani akisisitiza kuwa, shetani hamtakii mema mwanadamu hivyo aliwataka wana Mtwara kuwakataa wanasiasa wa aina hiyo.
“Hii gesi ni kwa ajili ya wakazi wa Mtwara, Ruvuma, Dodoma, Mbeya, Lindi, Dar es Salaam na mikoa mingine iliyopo nchini ikiwemo Zanzibar na dunia nzima kama ilivyo korosho ambayo inalimwa Mtwara lakini inauzwa duniani kote,” alisema.
Aliongeza kuwa, gesi iliyogundulika mkoani humo itapunguza gharama za umeme kwa kiasi kikubwa ambapo Shirika la Umeme nchini (TANESCO), litanunua gesi kwa shilingi tatu ambapo wananchi watanunua kwa shilingi tano.
Mchungaji Mwamalanga alisema, hivi sasa gharama za umeme ni kubwa hivyo ni vyema wanasiasa wajitambue kuwa uchochezi wao unarudisha nyuma maendeleo na kukwamisha uzalishaji.
Kwa upande wake, mkazi mmoja wa Newala ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema yeye alikuwa akitumika kuandaa makundi ya uchochezi.
Alisema mtandao wa uchochezi huo ni mkubwa ukianzia kwa baadhi ya watu kutoka Dar es Salaam ambao wanashirikiana na baadhi ya Wazungu ili kupindisha ukweli wa rasilimali hiyo.
Alisema ipo mikutano ya siri inayofanyika usiku ili kuhamasisha vitendo vya uchochezi kwa wana Mtwara ili wagomee gesi yao isisafirishwe kwenda Mkoa wowote ukiwemo Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, elimu aliyoipata kutoka kwa Mchungaji Mwamalanga, imemhamasisha kueleza ukweli huo na kuomba elimu hiyo iendelee kutolewa kwa wananchi wengi zaidi ili wasiendelee kutumika katika vitendo vya uchochezi.
Wakat i huo huo, baadhi ya wafanyabiashara mkoani humo wamempongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa jitihada zake za kuufufua uchumi wa Mtwara.
Walisema Prof. Muhongo ni kiongozi anayetembea kwenye kauli zake ambao hivi sasa wameanza kuyaona matunda ambapo vijana wameanza kupata ajira na mzunguko wa fedha kuwa mzuri.
Kabwe Zitto
Wakati mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ukisubiliwa kwa hamu kuanzia Mei 22-23 mwaka huu, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Kabwe Zitto, ameibuka na kupinga uamuzi wa Serikali kutoa vitalu vya mafuta na gesi katika Bahari Kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini.
Taarifa aliyotumwa na Bw. Zitto kwa vyombo vya habari jana, ilisema Wizara hiyo imeandaa semina inayohusu sera ya gesi asilia na tayari imetoa nakala kwa lugha ya Kingereza.
Alisema Semina hiyo ni maandalizi ya bajeti ya Wizara hiyo lakini jambo la kushangaza wakati sera ya gesi asilia ipo katika rasimu, tayari Serikali imetangaza kugawa vitalu hivyo.
“Zabuni hii mpya ya vitalu vya utafutaji imetolewa wakati kuna maamuzi ya Bunge kuzuia ugawaji huu hadi sera ya gesi asilia na Sheria ya Gesi vikamilike.
“Haraka hii ya Serikali kugawa vitalu bila sera wala sheria inatoka wapi, uamuzi wa kugawa vitalu vipya bila kuwepo kwa sera na sheria mpya unapaswa kupingwa,” alisema.
VURUGU ZILIZOTOKEA JANUARI 27 MWAKA 2013 KULE MTWARA HAKUNA HATUA YOYOTE ILIYOCHUKULIWA LICHA YA UHARIBIFUMKUBWA WA MIUNDOMBINU KUHARIBIWA JE KAMA NI ELIMU ILIKOSEKANA JE BAADA YA KUELIMISHWA WAMEELEWA TUSEME HAKUNA MWENYE KUMBUKUMBU YA YALIYOTOKEA KULE NIGERIA JIMBO LA BIAFRA LILIPOTAKA KUJITENGA NINI KWAO KUMEGUNDULIWA MAFUTA MENGI YA PETROLI ILIPIGANWA VITA NA ZAIDI YA WATU MILIONI MOJA WALIKUFA WANA MTWARA WALA HAWAFANYI KITU KIPYA NI KU-COPY NA KU-PASTE YALE YALIYOTOKEA NIGERIA MWAKA 1967-1970 TUJIULIZE NI HATUA GANI ZILICHUKULIWA
ReplyDelete