JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
linawashikilia watu watano kwa kukutwa na milipuko hatari ya mabomu ambayo
walikuwa wakiimiliki kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema watuhumiwa hao
wamekamatwa katika msako unaoendelea jijini humo.
Alisema katika
msako huo, jeshi hilo limekamata nyaya 62 za milipuko
zikiwa zimefungwa betri
na vifaa vya kusababisha mlipuko ambavyo vyote vikiunganishwa, vitatoa mlipuko
mkubwa unaoweza kuangusha ghorofa, kuua na kuharibu mali.
Aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni Bw. Juma Khalifan (24), Bw. Ruben Patrick (26), Bi.
Happy Charles (28), Bw. Sadick Seif (32) na Bw. Idd Shabani (40) ambao
walikamatwa eneo la Kunduchi Mtongani baada ya jeshi hilo kupata taarifa za
raia mwema.
Alisema pamoja
na kukamata milipuko hiyo, pia wamekamata gari aina ya Noah yenye namba
T 772 BYC pamoja na pikipiki aina ya Bajaj yenye namba T959 BTE zilizokuwa
zikitaka kusafirisha milipuko hiyo kutoka nyumba kwa Bw. Seif.
“Mara nyingi
milipuko hii inatumika kwenye shughuli za uvuvi na migodini ila cha ajabu
zaidi, watuhumiwa hawa si wavuvi wala hawamiliki migodi,” alisema Kamanda Kova.
Aliongezea
kuwa, kutokana na hali hiyo jeshi hilo limepatwa na mashaka juu ya watu hao
kumiliki milipuko na wapi walikuwa wanaipeleka hasa ukizingatia kuwa, yapo
matukio mbalimbali yanayoendelea kutokea nchini.
Alisema
jeshi hilo linaendelea kuwahoji watu hao kabla ya kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment