18 May 2013

Wateja wamuua mganga wao


Na Mashaka Mhando, Tanga


 GANGA wa kienyeji mkazi wa Kijiji cha Masatu, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Jafari Omari (79), amefariki dunia baada ya kunyongwa na mteja wake ambaye naye aliuawa na wananchi wenye hasira.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Mei 13 mwaka huu, saa 12:00 jioni nyumbani kwa mganga huyo kijijini hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Constantine Masawe, alisema siku ya tukio hilo, mganga huyo alifuatwa na watu wawili wakitaka kupata tiba asili na yeye kuwaagiza kuku kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema vijana hao walikwenda kijijini kutafuta kuku na baada ya kumpata walirejea kwa
mganga ambapo wakati wakiendelea na matibabu, mke wa mganga aliyefahamika kwa jina la Bi. Njema Jafari, alishtuka kuona mmoja ya vijana hao akitoka ndani mbio.
“Yule mwanamke kuona kijana mmoja akitoka kwa mumewe akikimbia, aliingia ndani kuona kilichotokea na kumkuta mme wake akiwa ameuawa hivyo alipiga kelele.
“Kijana mwingine aliyekuwa ndani kwa mganga naye alitoka mbio lakini alikamatwa na kuanza kushambuliwa na wananchi hadi alipopoteza maisha,” alisema Kamanda Masawe.
Alimtaja kijana aliyeshambuliwa na kupigwa hadi kufa kuwa ni Patric Lema ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kilichopo Dar es Salaam, aliyekuwa akisoma masomo ya jioni, anayekadiriwa kuwa na miaka 27-30.
“Tunaendelea kumsaka kijana mwingine aliyekimbia ambaye amefahamika kwa jina moja la Mahiza...nimewaomba wananchi watoe taarifa mara wamwonapo ili aeleze mazingira ya tukio hili ambalo hadi sasa limekuwa na utata mkubwa,” alisema.
Kamanda Masawe alisema pia jeshi hilo linamshikilia mwendesha pikipiki ya bodaboda ambaye aliwapeleka watuhumiwa hao kwa mganga huyo kwani maelezo yake yatasaidia uchunguzi ambao wameuanza kuhusiana na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment