RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan
Mwinyi, amependekeza nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
zitangaze mapumziko ifikapo Novemba 30 kila mwaka ili kuongeza uelewa wa
wananchi juu ya masuala ya mtangamano.
Novemba 30,1993
ndiyo siku ambayo Kamisheni ya Utatu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ilizinduliwa na hatimaye kuzaliwa upya kwa jumuiya hiyo ambayo ilikufa mwaka
1977 ambapo hivi sasa tarehe hiyo huadhimishwa kama “Siku ya EAC” lakini siyo
siku ya mapumziko katika nchi wananchama.
Alhaj Mwinyi
aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wakati akizindua ripoti ya
utafiti wa kwanza wa Afrika Mashariki juu ya ushiriki wa raia katika mchakato
wa ushirikiano wa EAC.
Uzinduzi huo ulifanywa na Jukwaa la
Dira ya Afrika Mashariki (VEAF), ambayo imebaini upo ushiriki hafifu wa raia
katika mwenendo mzima wa mchakato huo.
“Nawahamasisha marais waliopo
madarakani kwa sasa, kuienzi siku hii ya Novemba 30, 1993, ambayo Tume ya Utatu
ya Afrika Mashariki ilizinduliwa Mjini Arusha, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
akiwemo,” alisema Alhaj Mwinyi.
Aliongeza kuwa, siku kama hiyo
wananchi pamoja na mambo mengine wanaweza kufanya shughuli mbalimbali yakiwemo
maonesho ya utamaduni, bidhaa za kilimo na viwanda katika majiji yote na
mipakani na mwisho ya siku wananchi watakuwa na uelewa juu ya jumuiya hii.
Sehemu ya ripoti hiyo ilisema kuwa,
ingawa kuanzishwa upya kwa jumuiya hiyo kulilenga iwe na misingi yake kwa
wananchi, matokeo ya utafiti huo umebaini kinyume chake.
“Theluthi moja ya watu kama wa
Tanzania na Kenya, hawajawahi kusikia juu ya mtangamano wa EAC, ilisema ripoti
hiyo ambapo wanachama wengine wa jumuiya ni Uganda, Rwanda, Burundi.
Akizungumza katika tukio hilo,
Katibu Mkuu wa zamani wa
EAC, Balozi Juma Mwapachu, alitaka
mwananchi wa kawaida wahusishwe ipasavyo katika mchakato wa mtangamano.
Alisema wana Afrika Mashariki
wanahitaji kueleweshwa zaidi kuhamasishwa zaidi na kuwafanya wawe wamoja,”
alisema.
Naye
Rolf Paasch ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika moja la Ujerumani la
Frieddrich- Ebert-Stifstung (FES), nchini ambalo ndiyo limefadhili uzinduzi na
utafiti huo, alitoa wito kwa wana Afrika Mashariki kufanya kila wanaloweza ili
kuhusisha raia katika mchakato mzima wa mtangamano.
No comments:
Post a Comment