MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali
amesema kuwa kuanzia sasa mashamba yote ya karafuu na minazi yaliyokuwa chini
ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati yatakuwa
yakishughulikiwa na Wizara ya Kilimo na Maliasili, ili kuondoa mvutano wa
kiutendaji baina ya wizara hizo mbili.
Balozi Seif alitoa uamuzi huo katika
Chuo cha Amali vitongoji Chake Chake Pemba wakati akizungumza na masheha wa
mikoa miwili ya kisiwani Pemba.
Alisema udhibiti wa mapato
yanayotokana na mazao yaliyomo kwenye baadhi ya mashamba ya Serikali yalikuwa
yakileta mgongano kutokana na mashamba hayo kushughulikiwa na Wizara mbili
tofauti.
Hivyo aliwaomba Masheha ambao maeneo
yao yamo mashamba ya
Serikali ya karafuu na minazi na hadi sasa hayajahakikiwa
watoe taarifa kwa Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Pemba au kiongozi yeyote
atakayewekwa kwenye kanda hiyo.
Akizungumzia suala la udhibiti wa
ukataji ovyo wa misitu,Balozi Seif aliwakumbusha Masheha hao kuhakikisha kwamba
wimbi la ukataji ovyo wa miti unadhibitiwa.
'Kijani ya Pemba tunataka ibakie
kama kawaida na hili litafanikiwa iwapo wana jamii pamoja na masheha
watashirikiana katika udhibiti wa ukataji ovyo wa misitu' alisisitiza Balozi
Seif.
Wakielezea changamoto zinazowakabili
baadhi ya Masheha hao walisema mazingira duni wakati wanapostaafu utumishi wao
pamoja na mfumuko wa hujuma wanazofanyiwa masheha limekuwa tatizo kubwa
linalopunguza ari ya utekelezaji wa majukumu yao.
Masheha
hao waliiomba Serikali Kuu kujenga mazingira yatakayowawezesha kupatiwa mikopo
ya vyombo vya usafiri ili kurahisisha kazi zao masuala ambayo Balozi Seif
aliahidi kwamba Serikali itayazingatia na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.
No comments:
Post a Comment