MBUNGE wa Peramiho kwa tiketi ya CCM, Jenista Mhagama , amemkingia kifua,
Rais Jakaya Kikwete, akitaka Bunge lisimfanyie tathmini kuhusiana na kauli yake
kuwa hali ya kifedha kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini ni nzuri, kauli
ambayo kambi rasmi ya upinzani bungeni, imedai inapingana na ripoti ya Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo imeonesha hali ya mifuko
hiyo kuwa ni mbaya
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana, wakati
akichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka wa fedha
2013/14.
Alisema kuwa kitendo cha kumpakazia
maneno Rais Kikwete, si jambo la
heshima hata kidogo na hata kama amesema kweli
au hapana tumwache afanye kazi.
“Hatuwezi kusema tumfanyie tathmini
Rais katika Bunge hili, hili si suala la heshima hata kidogo kwani baba hawezi
kutoa siri ndani ya nyumba yake, lakini Rais Kikwete ameeleza wazi kuhusu
mifuko hiyo, hili ni jambo la kumpongeza,” alisema.
Alisema anaipongeza Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii kwani inafanya kazi yake vizuri na kutaka viongozi wa mifuko
hiyo kuendelea kuchapa kazi bila kubabaishwa.
“Halima (Mdee) hapa tulipo kwenye
jengo hili limejengwa na mifuko hii, Chuo Kikuu cha UDOM wanaposoma wadogo zako
kimejengwa na mifuko hii, sasa mnaposema hamuoni kazi mnataka kurudisha nyuma
maendeleo?” alihoji.
Kwa upande wa ajira, alisema ni
lazima kijipanga kutafuta suluhu na si kubaki kufurahia wawekezaji katika nchi
yetu. Alisema kabla wawekezaji hawajafika nchini, waulizwe wataajiri vijana
wasomi wangapi, wataje vijana wa elimu ya kati wangapi na vibarua wangapi, ili
ijulikane.
Aliongeza kuwa Wizara inatakiwa
kuangalia hali ya wafanyakazi kwenye sekta binafsi, kwani wengi wao wanaajiriwa
bila kuwa na mikataba na migogoro mingi inatokea katika sekta hizo kutokana na
mishahara duni.
Awali kabla ya Mbunge, Mhagama
kuanza kuchangia msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Cecilia Paresso,
akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo, alisema mifuko hiyo ipo katika hali mbaya
kulingana na na ripoti ya CAG.
Alisema ripoti hiyo ya CAG ilionesha
mifuko ya hifadhi ya jamii iko katika hali mbaya kutokana na kudai zaidi ya
trilion 6.4 fedha ambazo hazilipiki.
“Mfano PSPF ilitoa kiasi cha
sh.bilioni 67 ambazo hazilipiki, ambapo moja ya kampuni ambazo zilipewa fedha
hizo zisizolipika ni pamoja na kampuni ya Tanpower Resources ya makaa ya mawe
inayomilikiwa Benjamin Mkapa na Daniel Yona, ambayo ilipewa sh. bilioni 5.4,”
alisema Paresso.
Aliongeza kuwa kauli ya Rais Kikwete
wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi kuwa hali ya mifuko
hiyo ni nzuri inaonekana kutofautiana na ripoti ya CAG ambayo inaonesha hali ya
mifuko hiyo ni mbaya.
“Kutokana na kauli hizo mbili ya
Rais na CAG wananchi wanamuamini nani? Ni nani anayetoa taarifa sahihi juu ya
mifuko hiyo? Tumwamini Rais au CAG? Upi ni ukweli!” Alihoji Paresso na kuongeza
kuwa serikali isitishe mara moja miradi ambayo fedha zake hazilipiki.
Naye Mbunge wa Viti maalumu
(CHADEMA) ,Christowaja Ntinda alisema kuwa serikali iache tabia ya kugeuza
mifuko ya hifadhi za jamii kama ATM yao ya kutolea fedha na kushindwa kulipa
madeni yao.
Imeandikwa na Grace Ndossa Gladness Theonest, Goodluck Hongo.
No comments:
Post a Comment