15 May 2013

Ilani CCM yaleta mpasuko

Na Suleiman Abeid, Kahama


 MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mk o a n i S h i n y a n g a , Khamis Mgeja amekataa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya kwa madai imeandikwa ovyo na kwa dharau.
Mbali ya kukataa kupokea taarifa hiyo, Mgeja alilaani kitendo kilichooneshwa na mkuu huyo wa wilaya baada ya kubainika kuwa taarifa aliyopelekewa iliwahi kukataliwa pia hivi karibuni na
wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani Kahama.
Hata hivyo, kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo, Mpesya alikanusha kufanya dharau kwa chama chake na kwamba yeye anawajibika kwa Katibu wa CCM wilayani Kahama na siyo kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa na iwapo taarifa hiyo ilikuwa na mapungufu basi ndivyo ilivyoandaliwa na watendaji wake wa CCM.
“Nikiri ni kweli taarifa hiyo mimi ndiye niliyeipeleka kwa katibu wa CCM wa wilaya ambaye ndiye ninayewajibika kwake na siyo kwa mwenyekiti wa CCM wa mkoa, aliyepaswa kuipeleka kwake ni katibu wake wa CCM siyo mimi hivyo makombora niliyorushiwa yalistahili kuelekezwa kwa katibu huyo,” alieleza Mpesya.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Malunga wakiwemo wanachama na viongozi wengine juzi, Mgeja alisema CCM haitokubali vitendo vya kipuuzi vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali.
“Nimesikitishwa sana na kitendo cha mkuu wa wilaya, niliomba nipatiwe taarifa ya utekelezaji wa ilani yetu ya uchaguzi upande wa utoaji mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake, lakini nilicholetewa kimenishangaza, kinaonesha wazi mwenzetu huyu anatudharau viongozi wa chama,”
“Taarifa aliyoandika haiwezi kuandikwa hata na DC (mkuu wa wilaya) anayejifunza kazi, sijui mwenzetu huyu kiburi hiki anakipata wapi, nimeikataa na ninaomba iandikwe nyingine ikiwa na uchambuzi kamili kuonesha jinsi gani vijana na wanawake wamesaidiwa kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri,” alisema Mgeja.
Mgeja aliwataka watendaji wote wa serikali mkoani Shinyanga kuhakikisha hawafanyi vitendo ambavyo vitasababisha wananchi wakichukie chama chao hivyo kusababisha mpasuko wakati wa uchaguzi.
Kutokana na hali hiyo Mgeja aliahidi kupeleka nakala ya taarifa hiyo makao makuu ya chama na kwa Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga ili waweze kuona wenyewe madudu yanayofanywa na watendaji wa chini yao.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Kata ya Isaka aliyekaribishwa katika kikao hicho, Gavana Ally alishauri vikundi vyote vya vijana na wanawake wilayani humo kuandaa taarifa zao mapema zikionesha misaada au mikopo yote waliyokwishapokea kutoka halmashauri ili ilinganishwe na ile itakayoandikwa upya na mkuu huyo wa wilaya.

1 comment:

  1. Hili ndilo tatizo la kutofanya planning au kuifanya kisiasa. Rais ni mwana siasa na anapotoa ahadi, yeye anasema kisiasa. Ni kazi ya wataalamu kuitafsiri kauli hii. Kilichotokea hapa, Rais kasema na wataalamu wanamtarajia atekeleze mwenyewe; wapi na wapi. Wamemwaibisha.

    ReplyDelete